Dar/mikoani. Mlipuko wa bomu uliotokea Arusha
na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi 70 limezua utata
kutokana na hisia tofauti za viongozi mbalimbali nchini waliozungumzia
suala hilo, huku Rais Jakaya Kikwete akisema haamini kama Watanzania
sasa wamefikia hatua ya kuanza kuhasimiana kwa misingi ya kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Jiji la Arusha
kushambuliwa kwa bomu baada ya lile lililorushwa kwenye Kanisa la
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi kwenye Parokia ya Olasiti wakati
wa sherehe ya uzinduzi wake Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu na
kujeruhi 64. Wakati Rais Kikwete akisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wamesema
tukio hilo ni la kisiasa na lilipangwa.
Kufuatia tukio hilo, uchaguzi wa kata nne za Arusha mjini umeahirishwa hadi Juni 30.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana imeeleza kuwa
Rais Kikwete ambaye yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa nchi
zilivyoendelea kiviwanda(G8), alisema haamini kama Watanzania ama
wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kudiriki kufanya
matukio ambayo yanahatarisha usalama wa watu.
“Mimi siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa
vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa
aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema
nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki
miongoni mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye
machafuko makubwa.”
Mbowe
Akizungumzia suala hilo, Mbowe alisema shambulio
hilo la bomu ni la kisiasa na lililenga kumuua yeye na Mbunge wa Jimbo
la Arusha, Godbless Lema.
“Haya ni mauaji ya kisiasa ya kupanga, tumeokota
maganda ya risasi za bastola na SMG na tumepiga picha na kuwapa polisi
katika eneo la tukio, gari letu lilipigwa mlango na vioo kwa risasi na
kesho wabunge wote wa Chadema watakuwa hapa Arusha na wataondoka baada
ya mazishi,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema pia wamebaini bomu lililorushwa ni
la kiwandani na shambulizi hilo liliandaliwa na kikosi cha watu wengi
wenye lengo la kufanya mauaji makubwa.
Alisema kilichomwokoa na kifo ni kushuka jukwaani
saa 11:43 kabla ya muda wa kawaida wa saa 12:00 kwani ilipangwa
washambuliwe wakiwa juu ya jukwaa.
“Tunasikitika sana, watu wamekufa wasio na hatia
na msiba huu utakuwa wa kitaifa na tunatarajia kuaga miili katika uwanja
huohuo wa Soweto,” alisema Mbowe.
Profesa Lipumba
Kwa upande wake, Profesa Lipumba alisema watu waliohusika kulipua bomu walipanga kuvuruga uchaguzi huo uliyokuwa ufanyike jana.
Alisema CUF walikuwa na nguvu katika baadhi ya
maeneo ya uchaguzi Arusha ndiyo mana watu wameamua kuvuruga uchaguzi
ili usifanyike.
“Sisi tumewasimamisha wagombea udiwani ambao ni
Abbas Mkindi, (Kaloleni), John Bayo (Elerai) na Labora Ndarvio (Themi)
na maeneo haya tulitegemea leo (jana) tushinde ila baadhi ya watu
wameamua kuvuruga kwa malengo yao binafsi,” alisema Lipumba.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba amevitaka
vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliohusika na
milipuko hiyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nchimbi na Mwema
Wakati viongozi hao wakigawanyika Waziri wa Mambo
ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi na Inspekta Jenerali wa Polisi(IGP), Said
Mwema wamesema tayari jeshi lake limetuma timu inayoongozwa na Kamishna
wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Kamishna wa Idara ya
Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Dk Nchimbi
alisema uchunguzi wa awali umebaini ya kwamba bomu hilo ni la kurusha
kwa mkono (hand grenade).
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema hadi sasa hakuna mtuhumiwa yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
“Uchunguzi wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni
la kutupa kwa mkono. Tunachunguza kujua mlipuko ule ni wa aina gani,”
aliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha.
Dk Nchimbi alitaja orodha ya vifo katika tukio
hilo na kusema hadi sasa watu wawili wamethibitishwa kufa, huku 70
wakiwa wamejeruhiwa ambapo kati ya majeruhi hao, wawili wako katika hali
mbaya. Alisema kwamba uchunguzi huo unalishirikisha Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) ili kubaini mlipuko uliojitokeza ni wa namna gani.
Naye IGP Mwema alisema jeshi litaendesha
operesheni kali popote nchini ya kuwasaka na kuwatia mbaroni wote
waliowezesha, kufadhili na waliotenda uhalifu huo. Alisema Jeshi la
Polisi linalaani tukio hilo linaloashiria vitendo vya kigaidi ambalo
limesababisha vifo na majeruhi pamoja na kujenga hofu kwa wananchi.
“Nawashukuru wananchi walioanza kutupa taarifa za mwonekano, wajihi wa mtu aliyetupa bomu hilo,” alisema.
Mwema aliweka hadharani simu yake ya mkononi yenye namba 0754 785557 akitaka wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando (Dar), Mussa Juma na Moses Mashalla (Arusha).
No comments:
Post a Comment