Monday, June 17, 2013

MAPENZI YA JINSIA MOJA YADAIWA KUSHAMIRI HALMASHAURI YA MOROGORO



HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro inakabiliwa na changamoto ya kukua kwa maambukizi ya Ukimwi, baada ya kushamiri kwa biashara ya mapenzi ya jinsia moja. Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Naibu Meya Manispaa ya Morogoro, Lidya Mbiaji, alisema kuwa kumekuwa na tatizo kubwa la kushamiri kwa vichocheo vya ngono, hali inayochangia kukua kwa kiwango cha maambukizi ya Ukimwi katika mkoa huo.

Pia alisema ongezeko la nyumba za kulala wageni nalo limekuwa kichocheo kikubwa cha kushamiri kwa biashara ya ngono zembe.

Aliionya jamii kuepukana na mila na desturi zinazochangia kuleta vichocheo vya kuongezeka kwa maambukizi ya ukimwi, ikiwemo ngoma za unyago zijulikanazo kwa jina maarufu la kunemwa pamoja na mabanda ya kuonyesha video ambayo nje yamekuwa yakionyesha mechi za soka, lakini ndani ya mabanda hayo huonyesha picha za ngono na kusababisha kuleta hamasa ya watu kufanya ngono.

Pia aliviomba vyombo vya habari kusaidia kuelimisha jamii namna ya kujiepusha vitendo vinavyochangia maambukizi ya ukimwi, kwani hali si shwari kutokana na makundi ya watu wanaofanya biashara ya ngono kuvamia Manispaa ya Morogoro.

Alisema hata kwa wasomi wa vyuo vikuu, hali pia si shwari, kutokana tafiti kuonyesha kuwa wana kiwango cha juu cha kufanya ngono zembe, hivyo kulitisha taifa kupoteza wasomi wake mara baada ya kumaliza masomo yao.

“Kumekuwa na makundi makubwa ya jamii yanayoingia katika hatari ya kupata maambukizi…ukiangalia kundi la wanafunzi, watu masikini na wanawake, hasa wajane changamoto hii inawagusa moja kwa moja,” alisema Mbiaji.

No comments:

Post a Comment