Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana jijini Dar es Salam, alisema yupo
Dar es Salaam na tangu mwaka 2010 hajasafiri kwenda nje kama
inavyoelezwa na baadhi ya watu kwamba amekimbia nchi.
“Uvumi huo ni wa wazushi ambao idadi yao inaelekea kuongezeka siku
hizi.Wazushi hawa wamefikia hata kuwazushia watu kadhaa wakiwamo wasanii
na wanasiasa kwamba wamekufa, wakati siyo kweli, sijui sababu za uzushi
huu,” alisema Askofu Kakobe wakati akijibu maswali ya mwandishi kwa
njia ya simu.
Alisema siku yoyote kabla ya Jumapili ya wiki hii atasafiri kwenda
kufanya mkutano mkubwa wa injili jijini Toronto nchini Canada.
Kwa zaidi ya mwaka sasa kumekuwa na uvumi kwamba, Askofu Kakobe
ameikimbia Tanzania na kwenda kuishi katika Jiji la Toronto, kufuatia
mazingira magumu nchini katika kutangaza neno la Mungu.
Wanaozusha uvumi huo wamekuwa wakieleza sababu kadhaa zilizomfanya
Askofu Kakobe kukimbia nchini kuwa ni kutokana na kukumbwa na mikasa
kadhaa.
Miongoni mwa mambo yanayotajwa ni kwamba Mwaka 2007, Kakobe alikumbana
na kikwazo cha kwanza baada ya serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,
kufanya upanuzi wa Barabara ya Sam Nujoma kutoka Mwenge kwenda Ubungo.
Barabara hiyo ilisababisha sehemu ya maegesho ya magari nje ya kanisa
lake lililopo Mwenge, jijini Dar es Salaam kumegwa. Maegesho hayo
yalikuwa yakisaidia waumini wa kanisa hilo kuegesha magari yao wakati
wakiwa kwenye ibada.
Mwaka 2010, kulitokea mzozo mkali kati ya Shirika la Ugavi wa Umeme
Tanzania (Tanesco) ambalo lilitaka kupitisha umeme wenye msongo mkubwa
wa KV 132 mbele ya kanisa la Askofu Kakobe.
Askofu Kakobe alilipinga zoezi hilo akidai licha ya madhara kwa waumini
wake, umeme huo mkubwa utasumbua mitambo ya Televisheni ya Holiness
aliyowaonyesha waandishi wa habari ambayo aliifunga kanisani hapo kwa
ajili ya kurushia matangazo ya kiroho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment