WAANDAAJI wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF),
wameandaa warsha na kongamano kwa waandaaji na watayarishaji wa filamu
35 wanaoshiriki katika tamasha hilo linalotarajiwa kuanza Juni 29 hadi
Julai 7 katika Ukumbi wa Kome Kongwe mjini Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mratibu
wa tamasha hilo, Martine Mhando alisema warsha hiyo itasaidia kuongeza
ujuzi katika kupiga picha, kuhariri filamu, kuigiza katika kamera,
uandishi wa habari za sanaa, watoto na utengenezaji filamu.
Alisema katika tamasha hilo linalodhaminiwa na Kampuni ya Zuku, Tonya
Lee Williams ambaye ni muigizaji wa kimataifa kutoka Uingereza,
atakuwa mmoja wa wakufunzi na atawasaidia waigizaji na waongozaji wa
filamu wa hapa nchini.
Mhando alisema tamasha hilo kwa mwaka huu litawavutia zaidi
washiriki, kutokana na ZIFF kujipanga na kufanya mabadiliko makubwa
mwaka hadi mwaka.
“Tunawaomba waigizaji hata ambao kazi zao hazijachaguliwa waje
kushiriki warsha hii, kwani ni fursa kwao kutangaza kazi zao ambapo
wanaweza kusaidiwa na Zuku katika kuzitangaza zaidi kimataifa,” alisema
Mhando.
Pia alibainisha kuwa kutakuwa na jukwaa la watoto, wanawake na
vijana, ambapo kutakuwa na filamu mbalimbali zitakazoonyeshwa kati ya
80 zilizochaguliwa, zikiwamo 15 za Tanzania.
Alisema mbali na warsha hizo, tamasha hilo pia linatoa nafasi kwa
wasanii wa filamu kutoka nchi mbalimbali kwa kazi zao kuingia kwenye
tuzo za ZIFF, ambazo zinatolewa kwa msanii aliyefanya vizuri ikiwemo
tuzo ya filamu bora, msanii bora na nyingine.
“Katika tamasha mwaka huu wasanii wengi watakuwepo kutoa burudani
kama Mrisho Mpoto na Mjomba Band, Skylight Band, Linah, Fid Q, Barnaba,
Jhikoman, Baby J, Mkubwa na Wanawe, pamoja na wasanii wengine wengi
kutoka nchi mbalimbali.
Mwisho.
|
No comments:
Post a Comment