SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amekiri kuwepo kwa vitendo vya
unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike katika
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na hivyo kukataa mwongozo wa mbunge
akisema hali iko hivyo.
Makinda alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati Bunge likiwachagua
wawakilishi wake katika mabaraza ya vyuo na SADC-PF, ambapo Naibu
Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliuliza swali hilo la
uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono.
Mwalimu alimuuliza mmoja wa wagombea, Murtaza Mangungu (CCM) kuwa
UDOM imekithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanafunzi
wa kike kuombwa rushwa ya ngono na baadhi ya wahadhiri wasio waadilifu.
Naibu waziri huyo alitaka kujua, Mangungu ataondoshaje kero hiyo kwa
wanafunzi wa kike chuoni hapo, endapo atachaguliwa kuwa mjumbe wa
baraza.
Katika majibu yake, Mangungu alisema kuwa atashirikiana na wenzake
kuhakikisha wanaondosha kero hiyo kwa wanafunzi wanaofanyiwa vitendo
hivyo.
Baada ya majibu hayo, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo (CUF),
aliomba mwongozo wa spika, akitaka swali na jibu hilo vifutwe akidai
italeta picha mbaya kwa UDOM.
“Mheshimia Spika, aliyeuliza swali ni kiongozi wa serikali, naibu
waziri, sasa jibu hili likibakia hivyo italeta sifa mbaya kwa UDOM kuwa
kuna vitendo vya rushwa ya ngono, naomba swali na jibu vifutwe,”
alisema.
Hata hivyo, katika kujibu mwongozo huo, Spika Makinda alisema kwa kifupi: “Hakifutwi kitu hapa, hali ndivyo ilivyo.”
Kwa miaka ya karibuni, UDOM imekuwa ikitajwa kwa sifa mbaya ya baadhi
ya wahadhiri wake kuwaomba wanafunzi wa kike rushwa ya ngono ili
wawape upendeleo katika ufaulu wao.
Inaelezwa kuwa wako baadhi ya wanafunzi wa kike waliofelishwa
mitihani na kutakiwa kurudia masomo au mwaka baada ya kugoma kutimiza
matakwa hayo ya rushwa ya ngono.
Pia wanafunzi kadhaa wa kike wa chuo hicho, wamekuwa wakihusishwa na
matukio ya biashara ya ukahaba katika maeneo mbalimbali ya starehe
mjini hapa, hasa wakati wa vikao vya Bunge.
Katika hatua nyingine, Spika Makinda alitangaza washindi wa uchaguzi
huo wa wawakilishi wa Bunge kwenye mabaraza ya vyuo na SADC-PF.
Alisema kuwa Mangungu anakuwa mjumbe wa baraza UDOM baada ya
kumshinda Pudenciana Kikwembe wa Viti Maalum (CCM), huku Jitu Vrajlal
Soni akipita bila kupingwa kuwa mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo Morogoro (SUA) baada ya mshindani wake, Dk. Peter
Kafumu kujitoa.
Wengine ni Pindi Chana wa Viti Maalum (CCM) ambaye alipita bila
kupingwa kuwa mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia
Mbeya (MUST).
Spika aliongeza kuwa Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM) atakuwa
mjumbe katika Jukwaa la Kibunge la nchi Wanachama Kusini mwa Afrika
(SADC-PF).
Katika mchuano huo, Jafo aliwashinda Leticia Nyerere wa viti maalum (CHADEMA) na Lolesia Bukwimba wa Busanda (CCM).
|
No comments:
Post a Comment