Wachezaji wa Nigeria wameshindwa kusafiri kuelekea Brazil kufuatia mzozo kuhusu malipo ya ziada ya wachezaji.
Timu hiyo ya Super Eagles, inatarajiwa kucheza
mechi yake ya kwanza siku ya Jumatatu, lakini wamesalia nchini Namibia
baada ya mechi yao ya kufuzu kwa kombe la Dunia.Wachezaji wa Nigeria, hawajafurahishwa na uamuzi wa kuwapa dola elfu mbili kila mmoja, baada ya timu hiyo kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na Namibia mjini Windhoek.
Wachezaji hao wamesisitiza kuwa shirikisho la mchezo wa soka nchini Nigeria ni sharfti iongeze fedha hizo maradufu kabla ya wao kusafiri.
Ripoti zinasema kuwa wachezaji hao wamesema kuwa hawawezi kusafiri kuelekea Brazil hadi mzozo huo utakapotatuliwa.
Kuna wasi wasi kuwa mabingwa hao wa Afrika huenda wakakosa kushiriki katika fainali za kombe la shirikisho, itakayo anza tarehe kumi na tano hadi tarehe thelathini mwezi huu.
Rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Nigeria NFF, Aminu Maigari, alifanya mazungumzo na wachezaji hao jana usiku mjini Windhoek, kuwaeleza kuwa shirikisho lake halina fedha na ndio sababu malipo hayo ya ziada yalipunguzwa.
Wachezaji hao walitaka kulipwa dola elfu kumi kila mmoja kufuatia ushindi huo, lakini maafisa hao wa NFF walikataa pendekezo hilo.
NFF ambayo kwa sasa inakabiliwa na matatizo ya kifedha imelazimika kupunguza matumizi yake, likisema lilitumia kiasi kikubwa cha fedha zake katika fainali za kuwania kombe la mataifa ya Afrika iliyoandliwa nchini Afrika Kusini.
Nigeria ilikuwa imetangaza kuwa huenda ikajiondoa kwenye michuano ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki ligi ya nyumbani CHAN kutokana na matatizo ya kifedha.
Lakini uamuzi huo ulifutiliwa mbali baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia kati.
Wachezaji hao walitarajiwa kusafiri hadi Johannesburd leo kabla ya kuelekea nchini Brazil.
No comments:
Post a Comment