Habari za uchunguzi wa gazeti hili zimebaini kuwa msichana huyo, Pepetua Nyambura Maina (pichani), inadaiwa aliuawa na mfanyakazi mwenzake Philemon Laizer (27) ambaye pia alikuwa akimtumikia Jaji Kileo.
MAPENZI YATAJWA
Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa ni mtunza bustani katika nyumba ya Jaji Kileo na ilidaiwa kuwa wawili hao walikuwa na uhusiano wa siri wa kimapenzi lakini siku za hivi karibuni wakawa hawaelewani.
“Walikuwa marafiki wakubwa na inawezekana kijana alipoona msichana hamtaki tena, akaamua kumchinja. Ni uamuzi wa kikatili lakini ameufanya na kutuacha tumeduwaa,” kilidai chanzo.
Kijana Laizer anayedaiwa kufanya unyama huo ni Mmasai na alitiwa mbaroni na alipokaguliwa chumbani kwake, polisi walikuta nguo zilizolowa damu inayosadikiwa kuwa ni ya marehemu na wanaamini zililowa wakati anamchinja.
Licha ya nguo zenye damu, pia polisi walikuta kiatu kimoja ndani ya chumba chake ambacho kilikuwa kimevaliwa na marehemu kabla ya kuchinjwa.
Katika uchunguzi zaidi, habari zilidai kijana huyo alikutwa pia na nguo alizokuwa amevaa mrembo huyo wakati anakwenda kulala siku ya tukio zikiwa na damu.
“Polisi wanaamini kuwa Laizer alikuwa na wenzake, hivyo watuhumiwa wa mauaji haya ni lazima waongezeke,” kilidai chanzo chetu.
Habari za kina zinasema kuwa wawili hao walikuwa wanaelewana sana kiasi kwamba kwa yule ambaye alikuwa hajui angeweza kudhani kuwa walikuwa ni mtu na mdogo wake.
KINACHOSHANGAZA
Hata hivyo, kinachowashangaza watu ni kutosikia sauti yoyote ya kulalamika ya Pepetua kwani nyumba ya jaji ambayo wawili hao walikuwa wakiishi ipo karibu na nyumba za viongozi wa ngazi za juu serikalini na wengi wao wana walinzi kwenye mageti yao.
KOVA ANASEMAJE?
Akizungumzia tukio hilo, Kamishna Kova alikiri kukamatwa kwa Laizer akiwa na kiatu na nguo za marehemu pamoja na zake zilizokuwa na damu, huko maeneo ya Mikocheni B kulipotokea mauaji hayo.
“Tukio hilo lilitokea karibu na dampo la kutupa takataka Mikocheni ‘B’, katika eneo linalomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
“Mfanyakazi huyo wa ndani alikutwa ameshakufa baada ya mwili wake kuchinjwa sehemu ya shingo, jeraha sehemu ya mkono wa kushoto karibu na kiganja, jeraha kwenye paji la uso na mwili wake ukiwa umetapakaa damu sehemu za kichwani,” alisema Kova.
Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa akifanya kazi pamoja na marehemu, alikiri kuwa na marehemu siku hiyo ya Ijumaa ya Juni 8, mwaka huu.
“Baada ya mahojiano ya muda mrefu, alidai kuwa marehemu alitoweka nyumbani tangu Ijumaa na baada ya kubanwa na polisi mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo na atafikishwa mahakamani wakati wowote, ” alisema Kamishna Kova.
MWILI WAAGWA, WASAFIRISHWA
Mwajiri wa Pepetua, Jaji Kileo alimwaga machozi wakati wa kuuaga mwili nyumbani kwake Mikocheni B na baadaye ulisafirishwa kupelekwa kwao Naivasha, nchini Kenya kwa mazishi.
Habari hii imeandikwa na Makongoro Oging, Haruni Sanchawa na Issa Mnally
No comments:
Post a Comment