ASKARI 15 wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliofukuzwa kazi hivi karibuni kwa kosa la kupokea rushwa ili kupitisha mizigo bandarini kwa njia za magendo wameibuka na kutoa siri ya kufukuzwa kwao.
Mmoja
wa askari hao akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema sababu ya
kufukuzwa kwao imetokana na wao kukamata magari ya vigogo serikalini,
akiwemo aliyekuwa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
ambaye anadaiwa kuwa kinara wa kukwepa kodi.
Akizungumza
na gazeti hili, askari huyo alisema baadhi ya viongozi wa juu wa jeshi
hilo wamekuwa wakiwasaidia wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi na pindi
askari wadogo wanapoyakamata magari hayo hufukuzwa kama ilivyotokea
kwao.
Kwa
mujibu wa habari hizo, katika kesi ya kijeshi iliyotolewa hukumu ya
kuwaondoa kazini askari hao, waliomba waoneshwe dereva na gari
linalodaiwa kuwa lilitoa rushwa kwao kama kielelezo muhimu katika kesi
yao, lakini hadi sasa gari na dereva huyo hawajapatikana.
Mashtaka
ya askari hao, yalitarajiwa kusomwa na askari mmoja wa juu, lakini
alipobaini kwamba hakuna ushahidi, aliamua kujiondoa na kuchukuliwa na
askari mwingine ambaye ndiye aliyewasomea mashitaka.
“Baada
ya kesi kusomwa Juni sita mwaka huu, ikatolewa hukumu ya kutuondoa
kazini pasipo walalamikaji na vidhibiti kuwasilishwa katika mahakama ya
kijeshi. Kwa kifupi hatukutendewa haki na tunakusudia kukata rufaa,”
alisema askari huyo kwa niaba ya wenzake.
“Ukweli
ni kwamba wanaofanya baiashara ya kuingiza bidhaa bila kulipia kodi ni
viongozi wakubwa wa nchi hii hasa huyu kiongozi mstaafu wa Zanzibar na
mkewe, sisi leo hatupo kazini na wao wanaendelea kupitisha bidhaa
bandarini kwa rushwa,” alisema.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, akizungumzia hatua ya
askari hao kufukuzwa kazi alisema alichofanya ni kuthibitisha adhabu yao
baada ya kupitishwa katika kitengo cha nidhamu ya jeshi.
“Kwangu
si muhimu kujadili adhabu iliyotolewa na mahakama ya kijeshi,
nilichofanya ni kuthibitisha tu na kama wanaona wameonewa, tumewaambia
wakate rufaa,” alisema Wambura.
Akizungumzia
madai ya kuwalinda baadhi ya viongozi katika tuhuma za kusafirisha
mizigo pasipo kulipia ushuru, Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova, alisema yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo
aziwasilishe kwake.
Kuhusu
kukosekana ushahidi pamoja na wahusika waliotumika kutoa rushwa, CP
Kova, alisema hawezi kuwataja kwa kuwa walitumwa kuweka mtego wa
kuwanasa askari wanaosaidia watu kukwepa kodi.
No comments:
Post a Comment