MPANGILIO wa alama mpya za kufaulu kwa wahitimu wa kidato cha sita
waliohitimu mwaka jana, ambao matokeo ya mitihani yao yanaweza
kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, unadaiwa kuzua aibu na kama si
uamuzi uliotajwa bungeni wa matumizi ya alama za ufaulu za zamani,
matokeo hayo yangeibua aibu kama ilivyojitokeza kwa kidato cha nne,
2012.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka Baraza la
Taifa la Mitihani (NECTA) ambalo linaendelea kupanga matokeo hayo ya
kidato cha sita kwa kuzingatia alama za zamani kama ambavyo taarifa ya
awali ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilivyosomwa
bungeni hivi karibuni, hali ingekuwa mbaya zaidi katika ufaulu kwa
wanafunzi wa kidato cha sita kiasi cha kuweza kutishia uhai wa vyuo
vikuu nchini kukosa wanafunzi wa kutosha.
“Hali ilikuwa mbaya
sana kama alama za kufaulu zingeachwa zitumike zile mpya na si za
zamani. Vyuo vikuu nchini visingeweza kupata wanafunzi wa kutosha.
"Tatizo
hapa si uwezo wa wanafunzi moja kwa moja katika kumudu mitihani bali ni
kufanywa kwa mabadiliko ya alama bila kuwaandaa.
" Alama hizi
zilipaswa kuanza kutumika na wanafunzi wapya, yaani kama wanaanza kidato
cha kwanza wawe wanapewa mitihani ya kupimwa kwa kuzingatia alama mpya
na waendelee nazo hadi mitihano yao ya mwisho.
“Na hivyo hivyo
kwa wanafunzi wa kidato cha sita. Alama hizi mpya zinapaswa kutumika
kwako kuanzia wakiwa kidato cha tano mara wanapoanza shule, kila
mitihani wanayopewa isahihishwe na kupangiwa alama kwa kutumia hizi
alama mpya,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka NECTA.
Kwa
mujibu wa mabadiliko hayo ya alama, alama mpya zilizokuwa zimetumika
awali ni daraja F kuanzia 34 hadi sifuri; badala ya alama hiyo F kuanzia
20 hadi 0; daraja D kwa kuzingatia alama mpya linapaswa kuanzia 35
tofauti na awali, yaani alama 21.
Taarifa zaidi zinabainisha ya
kuwa, kati ya sababu za kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha
sita tofauti na muda uliotarajiwa yaani mwanzoni mwa Mei, ni pamoja na
upangaji upya matokeo hayo, ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa kwa kidato
cha nne ambapo matokeo yalitangazwa na kisha kufutwa ili kuyapanga upya
kwa kutumia alama za zamani.
Lakini alipoulizwa kuhusu masuala
hayo ndani ya NECTA, Ofisa Habari wa Taasisi hiyo nyeti nchini, John
Nchimbi alisema; “Kwa sasa niseme tu kwamba mchakato wa kuandaa matokeo
ya kidato cha sita unaendelea, siwezi kusema lini hasa utakamilika
lakini nina uhakika ni katika muda muafaka.”
Kuhusu matokeo ya
kidato cha sita kucheleweshwa kutokana kupangwa upya ili kupunguza idadi
ya waliofeli kutokana na matumizi ya alama mpya za kufaulu, Nchimbi
anasema; “Unajua haya maagizo haya ya bungeni (kupanga matokeo kwa
kuzingatia alama za zamani) yamekuja wakati mchakato wa kuandaa matokeo
ulikwishaanza. Kwa hiyo baada ya maagizo ilibidi kufanya kazi hiyo tena
kwa kufuata maagizo hayo.”
Hata hivyo, hakuweka bayana kama
matokeo ya awali kabla ya maagizo ya Serikali yaliyotolewa bungeni
kutumia alama za zamani yamewafanya wanafunzi wengi kufeli na badala
yake akasema; “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mchakato wa matokeo
hayo haukuwa umefika mwisho. Takwimu rasmi hazikuwa zimekamilishwa. Kwa
hiyo si sahihi kusema rasmi walifeli.”
Lakini wakati hali ikiwa
hivyo kwa upande wa matokeo yanayotarajiwa ya kidato cha sita, taarifa
zaidi zinabainisha ya kuwa, baada agizo la serikali la kufuta na
kurejewa upya kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012, takriban
wanafunzi 50,000 wamepata unafuu katika matokeo yao tofauti na awali.
Awali,
kwa kuzingatia matokeo ya kidato cha nne mwaka jana yaliyotangazwa
Februari, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa, jumla ya watahiniwa 126,847 tu kati ya
watahiniwa 397,136 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Katika
matokeo hayo idadi ya wasichana waliofaulu ilitajwa kuwa ni 46,181
wakati wavulana waliofaulu ikiwa wanafunzi 80,686 na idadi ya watahiniwa
wa kujitegemea waliofaulu ni 16,112 kati yao watahiniwa 61,001
waliofanya mtihani wasichana ni 6,7751 na wavulana 9,361.
Katika
matokeo hayo watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, daraja la
pili 6,453 na daraja la tatu ni 15,426, wakati waliopata sifuri ni
240,903 lakini kwa kuzingatia taarifa za vyanzo vyetu ndani ya Baraza,
idadi hiyo itabadilika kwa sababu ya alama kuongezwa kwa watahiniwa hao
wa mwaka 2012.
Lakini matokeo hayo yalitangazwa pamoja na vituko
walivyofanya baadhi ya wanafunzi, vikiwamo vituko vya kuandika matusi
kwenye karatasi za majibu ya mitihani na kutokana na makosa hayo,
watahiniwa 789 walifutiwa mitihiani yao.
No comments:
Post a Comment