In Summary
WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa kuwa kocha wa
Real Madrid, Jose Mourinho atatua Chelsea, Julai Mosi, hiyo inamaanisha
Rafa Benitez atalazimika kupishana naye mlangoni.
WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa kuwa kocha wa Real Madrid,
Jose Mourinho atatua Chelsea, Julai Mosi, hiyo inamaanisha Rafa Benitez
atalazimika kupishana naye mlangoni.
Hata hivyo miezi sita ya Benitez pale Chelsea
imekuwa na maana kwenye klabu na huenda jambo hilo likamfanya kocha mpya
apate mteremko.
Kwanza alitua kwenye klabu hiyo huku kila shabiki
akikunja sura kuashiria kuwa hawakupenda kumuona kocha huyo hasa kwa
kuwa kuna historia mbaya kati ya Chelsea na Liverpool aliyokuwa
akiifundisha zamani.
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, alifumba
macho na kumpa kazi kocha huyo licha ya kwamba mashabiki walikuwa bado
wanamkubali Roberto Di Matteo.
Sasa kocha huyo anakaribia kuondoka kwenye klabu
yake huku akiwa ameacha mtazamo tofauti, timu ambayo ilikuwa haina
uhakika wa kutua kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya sasa inakaribia kutua
hapo, timu imetua kwenye fainali ya Ligi ya Europa na kikosi chake si
cha mchezo kwani kinaweza kuitibulia safari timu yoyote kubwa. Kocha
huyo ametoa mapinduzi kwa kufanya haya;
David Luiz kuwa kiungo
Kabla ya msimu huu David Luiz alikuwa akicheza nafasi ya beki, lakini Benitez aliamua kumpa nafasi ya kiungo.
Mchezaji huyo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimudu nafasi hiyo na hivyokuifanya timu ichangamke zaidi na kupata mafanikio haraka.
Jambo hilo limetoa mwanya kwa mchezaji huyo mwenye
umri wa miaka 26 kujaribu kufunga kwa umbali mrefu, mfano mzuri ni
wakati alipofunga bao kwenye mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Europa
dhidi ya Basel na pia aliwahi kufunga bao la mita 30 kwenye mechi dhidi
ya Fulham msimu huu.
Awali mchezaji huyo alionekana hana kiwango kikubwa akiwa nyuma, lakini kwa wakati huu amekuwa tishio.
Torres ameanza kukubalika
Ingawa Fernando Torres hajafikia kiwango chake cha
siku za nyuma, angalau Benitez amemsadia na kuanza kurudisha chenji
kufuatia kusajiliwa kwa ada ya pauni 50 milioni kutoka Liverpool na kushindwa kutamba.
Torres na Benitez wote ni raia wa Hispania labda hiyo ndiyo ilifanya kocha huyo afahamu mchezaji huyo anatakiwa kucheza vipi.
Msimu huu mchezaji huyo amefunga mabao 21 kwenye
mechi 60, tofauti na msimu uliopita ambapo alifunga mabao 11 pekee.
Torres hajafanya vizuri sana, lakini angalau amerudisha ari uwanjani.
Kaonyesha uthubutu
Ukweli ni kwamba wakati Roberto Di Matteo
alipotimuliwa kwenye kikosi Novemba mwaka jana, makocha wenye majina
makubwa hawakutamani kujiunga na klabu hiyo.
Mmiliki wa klabu alijaribu kutafuta makocha wazuri
lakini walikataa. Licha ya kumuahidi donge nono kocha wa zamani wa
Barcelona, Pep Guardiola kocha huyo alikataa kujiunga na klabu hiyo ya
bilionea huyo wa Russia.
Wengi walikuwa wakiogopa kufika na kutimuliwa na kibaya ni kuwa timu ilikuwa na wakongwe wengi na haikuwa na ubunifu mpya.
Lakini Benitez ameweka mambo sawa, na tayari
makocha wakubwa kama Jose Mourinho, Manuel Pellegrini na David Moyes
wanatamani kufika hapo. Sababu nyingine iliyofanya makocha waogope kutua
ni ukweli kwamba ulikuwa mwaka mgumu kwa Chelsea.
Timu ilikuwa kwenye mashindano ya Kombe FA, Kombe
la Ligi, Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi ya Europa na
Klabu Bingwa ya Dunia. Makocha walikuwa wakiogopa kutimuliwa baada ya
kukosa vikombe vyote.
Uvumilivu
Kocha huyo alionyesha nguvu kubwa baada ya
kudharau matusi ya mashabiki uwanjani. Wakati alipochukua timu mashabiki
walimchukia sana na kelele zao ziliwafanya hata wachezaji wakose ari
uwanjani.
Hata hivyo kocha huyo hakukata tamaa, aliendelea kuijenga timu na hakujibu mashambulizi ya mashabiki hata siku moja.
Kocha huyo pia alikuwa na matatizo nje ya uwanja. Amekuta
wachezaji wakubwa ambao walikuwa bora chini ya Mourinho. Wakongwe kama
John Terry na Frank Lampard walitamba siku za nyuma lakini kwa wakati
huu viwango vinaanza kupotea. Benitez alianza kwa kuwapunguzia mechi na
kutoa nafasi kwa damu changa.
Jambo hilo lilizua mzozo kwenye klabu lakini
Benitez alifumba macho na kuendelea na kazi yake. Kuna wakati Benitez
alijaribu kuwaambia Lampard na Terry kwamba wakati wao umepita na aliona
wazi kuwa uamuzi wa kuwapanga Oscar, Juan Mata na Eden Hazard ulikuwa
sahihi kwake.
No comments:
Post a Comment