Tukio la kutupwa bomu katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi,
Arusha limetua katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) baada
ya kuwasilishwa na Balozi wa Vatican UN, Askofu Mkuu Frances Chullikatt.
Askofu Chullikatt anakuwa kiongozi wa kwanza wa Vatican kutoa tamko
kuhusiana na shambulizi hilo ambalo mmoja wa viongozi wake alikuwapo.
Bomu
hilo lilirushwa katika kanisa hilo wakati likizinduliwa na Balozi wa
Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla Mei 5, mwaka huu na
kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi zaidi ya 50. Wakati wa
shambulizi hilo, Askofu Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha,
Josephat Lebulu walionusurika.
Akihutubia Kikao cha Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani juzi, Askofu Chullikatt
alisema tukio lililotokea Arusha linadhihirisha kuwa kuna umuhimu ya
kupambana na ugaidi katika Afrika ili kuimarisha amani na usalama wa
kimataifa.“Unahitajika mshikamano na ushirikiano wa pamoja wa mataifa
mbalimbali katika kuchukua hatua za maisha na kulinda haki za binadamu,”
alisema Askofu Chullikatt, ambaye amekuwa mwakilishi wa Vatican kwenye
Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2010.
Askofu Chullikatt, ambaye ni
mzaliwa wa India, alisema suala la ugaidi linahitaji kuzuiwa duniani
kote na hasa Afrika kutokana na matukio hayo kuharibu maisha ya binadamu
na kutokea katika maeneo wanayofanyia ibada. Askofu Chullikatt alisema
pale ugaidi unapofanyika kwa kutumia dini, waumini na viongozi wao ni
lazima wahakikishe wanapambana nao ili kuutokomeza.
Alisema suala
la ugaidi linahitaji viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini kulilaani
kwani ni la kikatili katika maisha ya binadamu hivyo si vyema kukaa
kimya suala hilo linapotokea. Askofu Chullikatt alisema ugaidi unaotokea
Afrika unatakiwa kuangaliwa kimataifa ili kuzipa uwezo nchi hizo
kupambana na kuzuia matukio hayo.
Shambulio la bomu dhidi ya
kanisa la Arusha lilikuwa tukio la pili la ugaidi uliolenga kushambulia
wageni nchini. Mara ya kwanza ilitokea mwaka 1998, wakati Ubalozi wa
Marekani nchini ulipolipuliwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu kumi
na moja huku 85 wakijeruhiwa.
No comments:
Post a Comment