MOTO WAUA WATU WANNE WA FAMILIA MOJA JIJINI MWANZA ......BAADA YA KULA DAKU WALISAHAU KUZIMA JIKO
WATU
wanne wa familia moja, wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya
nyumba waliyokuwa wakiishi, kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.
Ajali
hiyo ilitokea eneo la Lumala Mashariki wilayani Ilemela na ilitokana na
jiko la mafuta, ambalo halikuzimwa baada ya wanafamilia hao kula daku
usiku; matokeo yake, lililipuka alfajiri.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, ndani ya
nyumba hiyo kulikuwa na pikipiki iliyokuwa na mafuta ya petroli, ambayo
ilishika moto na kuungua na kuteketeza watu waliokuwa ndani pamoja na
nyumba.
Waliokufa ndani ya nyumba hiyo, mali ya Fadhil Nuru, ni Amina Musa (75) na Mariam Musa (72) ambao ni mtu na dada yake.
Wengine
ni Busharat Bashir (23) na Janat Abdul mwenye umri wa miezi sita, ambao
ni mtu na mwanawe. Majeruhi, Dotto Twaa mwenye umri wa kati ya miaka 17
na 18, amejeruhiwa vibaya usoni, mkononi na kifuani na amelazwa katika
Hospitali ya Rufaa Bugando.
Taarifa
kutoka kwa ndugu wa marehemu hao, zinasema Mariam alikwenda kumtembelea
dada yake huyo, Amina, aliyekuwa akiishi kwa mwanawe. Busharati na
mwanawe, Janat, waliokuwa wakikaa Kirumba, walikwenda nyumbani hapo eneo
la Lumala, kumtembelea baba yao mdogo na kuwaona bibi zao hao, ambao
pia ni marehemu.
“Baba
ambaye ni mkuu wa familia, amenusurika. Yeye alikuwa amelala nyumba ya
mbele. Hawa waliokufa na huyo majeruhi, walikuwa wamelala nyumba ya
nyuma,” alisema mmoja wa wanafamilia, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini. Kamanda alisema,
Akizungumza
katika eneo la tukio, mmiliki wa nyumba hiyo, Fadhil Nuru alisema moto
ulioteketeza familia yake, ulizimwa na wananchi waliojitokeza
kuwasaidia.
Alisema walipiga simu mapema Zimamoto, lakini walichelewa kufika na kukuta tayari majirani wamezima.
“Kama
Zimamoto wangewahi kufika kusingekuwa na madhara makubwa ya kupoteza
wanafamilia wengi namna hii, hata hivyo nawashukuru wananchi kwa
kunisaidia,” alisema.
No comments:
Post a Comment