Marekani imeitaka Rwanda kuacha kusaidia waasi wa kundi la M23 ambalo linaendesha mapambano dhidi ya Serikali ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Taifa hilo kubwa duniani limesema lina ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa Rwanda inalisaidia kijeshi kundi hilo la waasi na baadhi ya maofisa wake wamo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kutoa kauli kali tangu kundi hilo lianzishe mapigano dhidi ya Serikali ya DRC katika mji wa Goma ulioko eneo la Mashariki, ambalo lina utajiri mkubwa wa madini.
"Tunaitaka Rwanda iache mara moja kutoa msaada wa aina yoyote kwa M23," alisema Jen Psaki, Msemaji wa Ikulu ya Marekani. Msemaji huyo pia aliitaka Rwanda iondoe wataalamu wake wa kijeshi ndani ya M23.
Marekani imetoa agizo hilo zikiwa zimebaki siku mbili kwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, John Kerry kuongoza kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) ambacho kitajadili masuala ya Afrika hasa amani ya eneo la Maziwa Makuu.
Kundi la M23 lilianza kuteka baadhi ya maeneo Mashariki mwa DRC mwanzoni mwa mwaka jana, huku likiishutumu Serikali kwa kushindwa kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2009.
Ripoti ya UN Juni mwaka huu, iliitaja Rwanda kuisaidia M23 ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa kundi hilo.
Pia ripoti hiyo inaeleza kuwepo kwa dalili za majeshi ya DRC kuwapa ushirikiano wapiganaji wa Kihutu wa kundi la FDLR ambalo linapambana na Serikali ya Rwanda.
Psaki alisema wasiwasi mwingine juu ya M23 unatokana na ripoti ya Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu Human Rights Watch, ambalo limedai kuwa na ushahidi wa namna kundi hilo linavyojihusisha na vitendo visivyo vya kibinadamu ikiwemo ubakaji na kulazimisha watoto kujiunga na kundi hilo linalopata msaada wa Rwanda.
Rwanda, hata hivyo, imekanusha madai hayo na kudai kuwa ripoti hiyo haina ukweli wowote. Pia imelaani shirika hilo la haki za binadamu kuwa linatoa madai wakati halina ushahidi.
Kuwepo kwa mapigano kati ya kundi hilo na majeshi ya Serikali kumeilazimu UN kupeleka majeshi ya kulinda amani katika eneo hilo la Mashariki mwa DRC.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopeleka jeshi lake chini ya mwavuli wa UN katika eneo hilo ambalo limetawaliwa na vita kwa miongo kadhaa sasa.
Human Rights Watch linasema M23 imeua zaidi ya watu 40 na kubaka zaidi ya wanawake na wasichana 60 tangu Machi.
Baada ya kuhoji zaidi ya watu 100 katika eneo hilo, shirika hilo lilisema waasi hao wanasajili kwa nguvu vijana wa DRC na wengine Rwanda.
Shirika hilo liliongeza kuwa Jeshi la Rwanda bado linawasaidia moja kwa moja waasi hao licha ya serikali ya Rwanda kupinga hilo mara kwa mara.
Wakati huo huo, Jeshi la DRC juzi lilishambulia ngome za waasi hao karibu na Goma yakiwa ni mashambulizi ya kwanza tangu vita kati ya pande hizo mbili kuanza Jumatatu asubuhi na kusitishwa siku hiyo mchana.
Kundi hilo lilisema liko umbali wa kilometa nne kutoka Goma, ingawa linasema lengo ni kulazimisha Serikali ifanye mazungumzo nao wala si kuteka mji wa Goma.
M23 iliteka mji huo kwa siku 10 Novemba mwaka jana, kabla ya kuondoka mjini humo kwa shinikizo la jumuiya ya kimataifa ili kufanya mazungumzo na Serikali ya Rais Joseph Kabila.
Mazungumzo na Serikali yalianza Kampala, Uganda Desemba mwaka jana na baada ya miezi miwili Jeshi lilianza tena mapigano na waasi hao Julai 14. Kulingana na UN mapigano hayo yalisababisha takriban watu 4,200 kutoroka kwao.
No comments:
Post a Comment