Kitendo cha Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa juzi, kimetafsiriwa kwamba ni kumfanya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kukalia kuti kavu. Kwa ushindi wake huo, Chadema kimefikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha wakati CCM kimebakiwa kuwa na viti 12 wakati TLP ina viti sita.
Pia Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti zaidi
kwani ina nafasi moja ya viti maalum iliyokuwa ikishikiliwa na Rehema
Mohamed aliyetimuliwa mwaka 2011.
Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema, Isaya Doita
alisema jana kwamba ushindi wa juzi ni chachu katika msimamo wa chama
chao kutaka uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha urudiwe akiamini kuwa
alichaguliwa kimizengwe.
Doita ambaye ni Diwani wa Ngarenaro, alisema wana
imani muda si mrefu Jiji la Arusha sasa litapata Meya ambaye
amechaguliwa kwa misingi ya sheria.
Chadema ilitetea viti vya Kata za Themi,
Kimandolu, Kaloleni na Elerai ilivyovipoteza baada ya kuwafukuza
waliokuwa madiwani wake kwa kosa la kukiuka maagizo ya Kamati Kuu ya
chama hicho kuhusu mwafaka wa umeya.
Ushindi huo unakihakikishia wingi wa wajumbe
katika baraza hilo la madiwani hivyo kuwa na fursa kumwondoa madarakani
Meya Lyimo. Doita aliahidi kuwa chama hicho kitakaa leo kutoa msimamo
kuhusu suala hilo la umeya wa Arusha.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa
Arusha, Mary Chatanda alisema Chadema kisahau suala la kuchagua meya
mpya kwani uchaguzi wake ulishapita.
Chatanda, ambaye pia anaingia katika vikao vya
Baraza la Madiwani la Arusha kutokana na kuwa Mbunge wa Viti Maalumu,
alisema Chadema kinapaswa kufanya kazi na meya wa sasa.
“Unajua vikao hivi vinaongozwa kwa kanuni, kwa
hiyo wingi wao si hoja ya kumvua meya au kulazimisha kupitisha mambo
yao,” alisema
Mamia wafurika Manispaa
Wabunge wanne wa Chadema jana waliongoza mamia ya
wafuasi wa chama hicho katika shamrashamra ya kuwasindikiza madiwani
wanne kwenda kujitambulisha kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.
Hata hivyo, furaha yao ilizimwa na polisi baada ya kumuomba Mbunge Arusha Mjini, Godbless Lema kuwatawanya.
Wabunge wengine walikuwa Mchungaji Israel Natse (Karatu), Joshua
Nassari (Arumeru Mashariki) na Grace Mukya (Viti Maalumu) ambao
walitokea ofisi za Chadema Mkoa wakiwa na wafuasi wa Chadema wakiwamo
vijana wa bodaboda, magari na watembea kwa miguu.
Wakati wabunge hao, wakiwa katika magari yao,
Madiwani wanne wa Chadema, walioshinda, Mchungaji Rayson Ngowi
(Kimandolu) Edmund Kinabo(Themi), Mhandisi Jeremiah Mpinga (Elerai) na
Kessy Lewi (Kaloleni), walikuwa katika gari la wazi.
Hata hivyo, walipofika katika eneo la Halmashauri
waliwakuta polisi wakiwa wametanda katika eneo hilo na kuwaruhusu
wabunge, madiwani na viongozi pekee kuingia. Agizo la Kamanda wa Polisi
Wilaya ya Arusha (OCD), Gillis Mrotto kuwataka wafuasi hao kutawanyika
halikufanikiwa hadi alipomuomba Lema kuwatawanya wafuasi hao.
Akizungumza na madiwani hao, Mkurugenzi Jiji,
Sipora Liana aliwaahidi ushirikiano: “Nawapongeza na naomba tushirikiane
katika kazi. Mimi kwa kawaida sipendi ubadhirifu.”
Mbowe ajisalimisha Polisi
Jeshi la Polisi Makao Makuu limemhoji Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe kwa madai kuwa kauli zake alizozitoa baada ya
kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho ni za uchochezi.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni alihojiwa kutokana na madai kwamba alisema polisi ndiyo
waliohusika na ulipuaji wa bomu Arusha, waliisaidia CCM kwenye uchaguzi
na kumtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuhusika na mauaji ya Arusha kutokana
na kukaa kwake kimya.
No comments:
Post a Comment