CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekuja juu na kuitaka Serikali kuangalia njia nyingine mbadala ya kukusanya kodi na kuachana na mpango wa kuanza kuwatoza wananchi tozo ya Sh 1,000 kila mwezi kwa kila laini ya simu ya kiganjani.
Hatua hiyo, inatokana na kilio cha wananchi ambao tangu Bunge la Bajeti kwa mwaka 2013/14 kupitisha sheria hiyo, kumekuwa na manung’uniko mengi.
Uamuzi huo, ulipitishwa na Bunge baada ya mjadala mkali pindi bajeti ilipotangazwa kitendo kilichomfanya Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa kuomba Serikali ipewe muda wa kutosha wa kujadili suala hilo.
Baada ya majadiliano na Kamati ya Bajeti ambayo inaongozwa na Mbunge wa Bariadi, Chenge Chenge (CCM), Waziri Mgimwa pamoja na Bunge waliridhia wananchi waanze kutozwa fedha hizo, kuanzia Julai mosi mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye mjini Dar es Salaam jana, ilisema CCM inapinga tozo hiyo kwa sababu itaongeza mzigo kwa mwananchi wa kawaida na kusababisha usumbufu usiokuwa na sababu kwa walalahoi.
Tozo hiyo, ilipitishwa na Bunge la Bajeti ikielezwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa kuibua vyanzo vipya vya kodi pale vinapoondoshwa vilivyopo kwa sababu mbalimbali.
Katika taarifa hiyo, Nape alisema licha ya umuhimu huo, vigezo vilivyotumika kupanga viwango sawia vya kodi hiyo kwa kila mtu mwenye laini ya simu, havijazingatia hali ya utofauti wa kipato kwa Watanzania.
Alisema wengi wao, matumizi yao ya simu ni ya kiwango cha chini mno tofauti na Serikali inavyofikiria.
"Kama chama tawala, tunaona hatuwezi kukaa kimya kwenye jambo ambalo tunaliona linawabebesha mzigo wananchi na huenda likarudisha nyuma maendeleo na kuchelewesha jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla," ilisema taarifa hiyo
No comments:
Post a Comment