Thursday, July 18, 2013

MEYA ARUSHA AWAVIMBIA CHADEMA "WANAOTA NDOTO ZA ALINACHA"


Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo (CCM), ametamba kuwa wanaofikiria kumng’oa kwenye kiti chake wanaota ndoto za alinacha kwa sababu lazima wazingatie kanuni za uendeshaji wa Mabaraza ya Madiwani.
Baada ya kushinda kata nne za Arusha kwenye uchaguzi mdogo juzi, Chadema ilitamba kuwa kazi inayofuata ni kumng’oa Meya kutokana na kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Madiwani.
Lyimo aliliambia Mwananchi kuwa pamoja na Chadema kuwa wajumbe wengi kwenye Baraza la Madiwani, bado hawana ubavu wa kumtoa.
Alisema ili kumtoa katika nafasi hiyo wanahitaji kuwa na theluthi mbili ya wajumbe . Lyimo alisema maana yake ni kuwa ili ang’oke lazima Chadema waungane na madiwani wa CCM ndiyo watafanikisha azma hiyo.
“Sharti la kumng’oa madarakani Meya au Mwenyekiti wa halmashauri ni kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote. Najiuliza wenzetu watafikiaje kiwango hicho hadi waanze kutamba kuning’oa madarakani,” alisema Lyimo.
Jiji la Arusha lina jumla ya wajumbe 32 kwenye Baraza la Madiwani ambapo ukimtoa Meya, wajumbe wanaostahili kupiga kura wanasalia 31 hivyo kufanya wenye nia ya kumng’oa kiongozi huyo kuhitaji zaidi ya kura 24 kutimiza lengo lao.
Baada ya kunyakua viti vyote vinne kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita, Chadema imefikisha wajumbe 15 kwenye baraza ikiwa ni madiwani 12 pamoja na wabunge watatu, wawili wa viti maalumu na mmoja wa jimbo.
Kwa upande wake, CCM kimebakia na wajumbe 14, ikiwa ni madiwani 11 na wabunge watatu wa viti maalumu, huku TLP ikiwa na wajumbe wawili ambao ni diwani mmoja wa kata na mwingine wa viti maalumu.
Kata ya Sombetini ambayo awali ilishikiliwa na CCM iko wazi baada ya aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo kujivua uanachama na kuhamia Chadema.
Kutokana na mchanganuo huo, Meya Lyimo alisema hana hofu ya kupoteza nafasi yake kwa sababu ili Chadema wafikie lengo hilo, ni lazima waungwe mkono na wajumbe kutoka CCM, jambo alilosema ni ndoto ya kutokea.
“Nakusisitizia ndugu yangu, mimi nipo na nitaendelea kuwepo hadi mwisho wa kipindi changu kwa uwezo na msaada wa Mwenyezi Mungu. Hakuna wa kuning’oa. Hata leo nilikuwa ofisini kutekeleza majukumu yangu ya kuongoza kikao cha kamati ya fedha,” alitamba Lyimo.
Meya huyo aliwataka madiwani kutoka Chadema kuacha kupoteza muda na nguvu nyingi kuweka mikakati ya kumng’oa madarakani, badala yake watumie muda na nguvu hizo kuwatumikia wananchi waliowaamini na kuwapigia kura kwenye uchaguzi.

No comments:

Post a Comment