Tuesday, July 30, 2013

BILIONEA WA SHOPPING CENTER ALIYEMWAGIWA TINDIKALI DAR… HALI TETE


HALI ni tete kuhusiana na tukio la bilionea Said Mohamed Saad kumwagiwa tindikali, athari ni kubwa. Jinsi alivyoharibika inatia simanzi lakini kumpata mhusika wa unyama huo ni kitendawili kinacholitega Jeshi la Polisi Tanzania

Rais Kikwete akimjulia hali mmiliki wa Kampuni ya Home Shopping Centre, Said Mohamed Saad.
Said ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni ya Home Shopping Centre, yenye maduka mengi makubwa ya vitu vya nyumbani ndani ya Dar es Salaam na mikoa kadhaa ya Tanzania, anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini lakini mmoja wa watu waliomshuhudia, amefafanua jinsi hali ilivyo mbaya.
“Ameungua sana, tunatarajia kati ya kesho au keshokutwa (wikiendi iliyopita) atafanyiwa oparesheni ya jicho. Jamani tindikali ni mbaya sana, usimmwagie mwenzako. Ndugu yetu ameharibika sana,” kilisema chanzo chetu kwa ombi la kutotajwa jina gazetini, kikaongeza:
“Kila anayemjua vizuri, anapomwona anamwaga machozi. Picha za jinsi alivyoathirika baada ya kumwagiwa tindikali zimevuja mpaka kwa familia, ni kilio kwa ndugu. Wanawake wanalia zaidi.”

JK ATINGA HOSPITALI
Wiki iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, alikuwa kwenye ziara ya kikazi nchini Afrika Kusini alipokwenda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini ya Afrika (SADC).
Mkutano huo ni wa Pande Tatu za SADC (Troika of SADC) na akiwa huko, alipata fursa ya kwenda kumjulia hali katika hospitali aliyolazwa ambayo haijajulikana jina.
Chazo chetu kilisema: “Rais Kikwete alisikitika sana. Wakati anatoka wodini alisonya. Alionesha jinsi alivyosikitishwa na unyama aliotendewa Said.”
Bilionea Said Mohamed Saad akiwa hospitali.
WAPELELEZI WAMWAGWA KARIAKOO
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Camillius Wambura aliwaambia waandishi wetu wiki iliyopita kwamba jeshi linaendelea kufanya kazi yake kuhakikisha linampata mhusika wa unyama huo.
“Mpaka sasa tuseme ukweli hatujampata mtuhumiwa au kitu kinachoonesha mtuhumiwa alivyo lakini kazi inafanyika. Tupo makini kwelikweli na tumeweka mkazo wa hali ya juu,” alisema Wambura.
Kwa upande mwingine, chanzo chetu ndani ya jeshi la polisi kimehabarisha kuwa idadi kubwa ya wapelelezi wamemwagwa Kariakoo, Dar es Salaam.
“Kuna mambo yanazungumzwa kuhusiana na tukio la Said kumwagiwa tindikali, yanafanyiwa kazi. Kutokana na ukweli kwamba msingi wa biashara za Said ni Kariakoo, vilevile kwa sababu inatambulika kuwa eneo hilo lina wafanyabiashara wengi, imebidi kulimulika kwa undani kabisa.
“Inawezekana ni chuki za kibiashara. Yaani aliyemtendea, ama alimshambulia au alifanya kulipa kisasi kutokana na vita ya kimaslahi. Hili suala tunaliangalia kwa upana sana ndiyo maana wapelelezi wamemwagwa Kariakoo.
“Wanachunguza kila taarifa. Kila kinachozungumzwa kinafanyiwa kazi na wale ambao itaonekana upo ulazima wa kuwakamata, watakamatwa ili kuisaidia polisi kufanikisha kumpata mtu ambaye alihusika na kummwagia tindikali yule bwana wa Home Shopping Centre,” kilisema chanzo chetu.

DAR YOTE INAPELELEZWA
Kwa mujibu wa chanzo chetu, pamoja na upelelezi kuwekewa mkazo Kariakoo lakini kazi ya kumsaka mhalifu aliyemfanyia unyama Said, inafanyika ndani ya jiji lote la Dar es Salaam pamoja na mikoa ambayo taarifa zitaelekeza.
“Kipindi chote ambacho upelelezi unafanyika, pengine zitaibuka taarifa zinazoelekeza mikoani ili kumpata mtuhumiwa, polisi watafika kote. Ukweli ni kwamba siyo tukio hili tu, jeshi la polisi limekuwa imara kufanyia kazi kila aina ya uhalifu.
“Pamoja na ugumu wa kumpata mtu hasa aliyemmwagia tindikali kutokana na mazingira yalivyokuwa, hilo halifanyi tukae kimya na tuache hili suala lipite. Maisha ya watu yanathaminiwa sana, unyama wa kuwadhuru wengine kwa vitu hatari kama tindikali, haukubaliki ndani ya polisi,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Maswali kuhusu aliyemmwagia tindikali hiyo, nani mhusika pamoja na sababu ya huyo aliyemmwagia tindikali, pengine ni mambo ambayo yanahitaji muda zaidi. Polisi wafanye kazi, mafanikio yake, yatatanzua utata wote.”

SHEMEJI MTU ATAJWA
Huku upelelezi ukiendelea, zipo taarifa kwamba mtu mmoja anayedaiwa kuwa shemeji wa Said, anatakiwa kuhojiwa kwani alishawahi kuripotiwa kuwa na uhusiano mbaya.
Ilibainishwa kwamba kumpata mhusika wa unyama huo, ni lazima kila aliyewahi kuripotiwa kuwa na tofauti za kijamii au kibiashara na Said, akamatwe na ahojiwe ili kuisaidia polisi.
“Yule shemeji yake ilishaelezwa waligombana sana. Mitandao ya kijamii ikaandika sana. Polisi hawatakiwi kudharau taarifa. Wamfuatilie huyo shemeji mtu, ahojiwe kwa makini,” alisema mfanyabiashara mmoja wa Kariakoo (jina tunalo), akaongeza:
“Siyo huyo shemeji yake peke yake, hata watu wengine wenye historia ya kugombana na Said, nao pia wamulikwe. Hili jambo ni nyeti, tena zito sana. Kumtenda binadamu ukatili wa kiwango hicho ni suala ambalo haliwezi kuvumilika.”

BODABODA TISHIO KWA NCHI
Said, alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu akiwa kwenye moja ya maduka yake katika Jengo la Msasani Mall, Dar ambalo nalo inadaiwa yeye ndiye analimiliki.
Taarifa za siku ya tukio zilibainisha kwamba Said alikuwa akizungumza na mfanyakazi wake mishale ya saa 1 jioni ndipo akatokea kijana mrefu, mwembamba ambaye alimmwagia kimiminika kinachosadikiwa kuwa ni tindikali.
Ilibainishwa kwamba mfanyakazi huyo wa Said, Hassan Ahmad naye alijeruhiwa kidogo katika purukushani hiyo lakini alipopelekwa Hospitali ya Ami Wellness Centre, alitibiwa na kuruhusiwa huku bosi wake akipelekwa Afrika Kusini usiku huohuo.
Kwa vile mtu aliyemmwagia tindikali Said alifika eneo la tukio na pikipiki, Kamanda Wambura (RPC Kinondoni), alisema kuwa uhalifu kwa njia ya usafiri huo ni mkubwa sana, kwa hiyo kuna taarifa inaandaliwa.
“Uhalifu wa pikipiki hususan bodaboda ni tishio kwa nchi yetu kwa sasa, kuna taarifa inaandaliwa na itatolewa baadaye kuhusiana na mwongozo wa usafiri huo pamoja na namna ambavyo kama nchi, tutakabiliana na uhalifu kwa njia ya bodaboda.
“Kwa sasa mamlaka husika zinakaa. Zinajadili, siyo suala la kupuuza kabisa. Majambazi sasa wanatumia pikipiki, tunashuhudia kwamba hata watu wanaotaka kutekeleza njama za mauaji, nao wanatumia bodaboda. Ni hatari sana,” alisema Wambura.

UWAZI LINAMWOMBEA APONE HARAKA
Gazeti hili, linamtambua Said kama mfanyabiashara na mlipa kodi wa nchi yetu ambaye mchango wake ni mkubwa katika kulipa afya taifa kwa upande wa mapato na bajeti yake kwa jumla.
Said, vilevile ni mhisani wa kijamii, kwani kupitia kampuni yake ya Home Shopping Centre, aliwasaidia sana waathirika wa mafuriko ya Bonde la Mto Msimbazi, mwaka juzi.
Mfanyabiashara huyo, aliipa kila familia seti ya vyombo vya nyumbani pamoja na taa zinazotumia nishati ya mwanga wa jua.
Familia hizo ambazo idadi yake ilikuwa 655, zilipohamishiwa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Said alijenga madarasa ya shule ya msingi kwenye eneo hilo ili kusaidia upatikanaji wa elimu na kurahisisha huduma za kijamii.

No comments:

Post a Comment