Friday, July 26, 2013

KIKWETE"ATAKAYE SUBUTU KUIGUSA TANZANIA ATAKAKIONA CHA MOTO"

Rais Jakaya Kikwete ametuma ujumbe kwa wale wanaoitishia Tanzania. Amewaambia wakithubutu watakiona cha mtemakuni kama ilivyokuwa kwa Idd Amin wa Uganda.
Alisema mamlaka za ulinzi na usalama zilimdhibiti Amin alipofanya uvamizi katika ardhi ya Tanzania mwaka 1978 na kwamba hazitashindwa kufanya hivyo kwa mtu mwingine yeyote atakayechezea usalama wa nchi.
Wakati Rais akisema hayo, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange amewahakikishia wananchi kuwa wakati wote jeshi liko imara na kuwataka wasiogope lolote.
Viongozi hao walisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa iliyofanyika katika Kambi ya Jeshi ya Kaboya iliyopo Muleba, Kagera.
“Sihitaji kusema tena, mmeshamsikia Mkuu wa Majeshi, atakayejaribu atakiona cha mtemakuni, laleni usingizi na msiwe na wasiwasi, msisikilize maneno ya mitaani,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Wakati wowote, saa yoyote tuko tayari kulinda nchi yetu. Hatuko tayari kuona amani inaharibika nchini, hatuwezi kuruhusu mtu yeyote kuimega au kuichezea nchi yetu kama alivyofanya Idd Amin.”
Katika siku za karibuni kumekuwa na kauli kadhaa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa nchi jirani ambazo zinatafsiriwa na wananchi kwamba ni za kuitisha Tanzania.
Jenerali Mwamunyange alisema jeshi wakati wote liko imara kuwalinda wananchi na nchi kwa jumla hivyo wasiogope...“Endeleeni na shughuli zenu na msiogope mtu yeyote, fanyeni kazi zenu bila wasiwasi.”
Huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria maadhimisho hayo, Jenerali Mwamnyanye alisema yeyote atakayethubutu kuchezea usalama wa nchi atakiona cha mtema kuni.
Akizungumzia Siku ya Mashujaa, Rais Kikwete alisema ni siku ya kuwakumbuka mashujaa waliojitolea maisha yao wakati wa Vita ya Kagera kuilinda nchi yao ili iwe salama na yenye amani.
“Kuhakikisha usalama wa nchi kuna gharama yake kwani kuna wengine walikufa na wengine wakabaki na vilema kwa ajili ya hilo. Wale ambao wamebaki na wana matatizo lazima tuwaangalie vizuri na vile ambavyo havijafanyika tutavishughulikia kwani kutetea taifa ni kazi ngumu.”
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu ambao wote walipewa nafasi ya kuwasalimia wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo.
Awali, viongozi wa dini, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba Methodius Kilaini, Shehe wa Mkoa, Haruna Kichwabuta na Mwakilishi wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo, Askofu Elisa Buberwa walitoa wito kwa Watanzania kuthamini amani iliyopo na umuhimu wa kuwa na mshikamano katika kuilinda na kuhakikisha kwamba haivurugwi kwa misingi ya imani, itikadi au ukabila.
Matatizo Muleba
Awali, Rais Kikwete aliwahakikishia wananchi wa Muleba kuwa matatizo ambayo wabunge wao wameyawasilisha kwake mbele yao atayashughulikia.
“Nimesikia yale waliyoyasema hapa ; suala la mpaka kati ya eneo la wananchi na jeshi, Waziri wa Ardhi yupo hapa, kaeni na jeshi na vijiji ili tatizo liishe ni jambo ambalo linawezekana hivyo litatuliwe,” alisema Rais Kikwete.
Alisema suala la umeme na madaraja litashughulikiwa na viongozi wa mkoa wakishirikiana na wabunge na watakapokwama wafikishe kwake... “Mimi ndiye ninayetoa fedha za maendeleo hivyo hayo masuala yakikwama waniambie nitayashughulikia.”
Imeandikwa na Boniface Meena Dar na Joas Kaijage, Muleba

No comments:

Post a Comment