Hili ni sakata la kikongwe mmoja anayedaiwa kumiliki idadi kubwa ya madanguro katika uwanja wake na kuwapangisha makahaba katika eneo maarufu kwa jina la Kijiji cha Makahaba.
Mwandishi wetu alipokea ujumbe mfupi ulioelezea ufuska unaofanywa na mabinti ambao hupewa eneo na kujenga vibanda kisha kujiuza kwa bei chee katika kijiji hicho maeneo ya Kigamboni jijini Dar.
Baada ya kujiridhisha na uchunguzi kuwa ni kweli jambo hilo linafanyika eneo hilo,waandishi walivamia eneo la tukio wakiwa na mjumbe wa mtaa huo aliyefahamika kwa jina la Abbas na kujionea madanguro yaliyojengwa kwa mstari ambapo milango yake iliachwa wazi huku ndani wakionekana mabinti wakiwa wamejilaza kihasarahasara wakiwatega wateja wanaopita katika mtaa huo.
Madanguro hayo ambayo kwa hesabu ni takriban kumi na nane, yamejengwa kwa aina yake ambapo mengi kati ya hayo yana ukubwa wa kutosha kuingia kitanda kidogo pekee.
Baada ya kujionea hayo, kikosi kazi sambamba na mjumbe huyo kilimtafuta mzee Matutu na kufanikiwa kuzungumza naye kuhusu madanguro hayo na namna anavyoyaendesha ambapo alikiri kuwa yeye ni mmiliki wa eneo hilo na huwa anapokea shilingi 30,000 kwa mwezi kwa kila mwanamke na fedha hiyo ndiyo inayomsaidia kuendesha maisha.
“Sina kazi nyingine ya kuniingizia kipato zaidi ya hii ya wasichana licha ya kwamba sijawaruhusu wafanye biashara hiyo. Fedha hiyo ndiyo inanisaidia kwa mahitaji yangu,” alisema kwa tabu mzee Matutu huku akimtaja msimamizi wa madanguro hayo kuwa ni mpwa wake.
Kwa upande wake mjumbe wa mtaa huo, Kassim alisema kuwa serikali ya mtaa imejitahidi kwa kadiri ilivyoweza kuwaondoa mabinti hao lakini wamekuwa wakirudi kila mara.
Alipoulizwa hatua waliyoichukua kwa mmiliki wa madanguro hayo ambaye ni mzee Matutu, kiongozi huyo alibakia kusikitika asijue hatua gani ya kumchukulia mzee huyo ambaye hata wakimpeleka kwenye vyombo vya sheria anahisi itakuwa ni uonevu kwa kuwa hana msaada mwingine wa kifedha zaidi ya fedha kutoka kwa mabinti hao.
No comments:
Post a Comment