Utamaduni wa taasisi nyingi hapa nchini wa kukataa kuwajibika
pale makosa yanapofanyika, badala yake lawama zikaelekezwa mahali
pengine pasipohusika, sasa unaonekana kama jambo la kawaida. Ni
utamaduni hasi wa kutokubali kuwajibika kwa jambo lolote linalokwenda
kombo, badala yake kuwanyooshea vidole watu wengine, tena ambao
hawahusiki katika kusababisha matatizo hayo.
Ni utamaduni huo ambao umefifisha dhana ya
uwajibikaji katika nchi yetu. Ni utamaduni unaojenga mazingira ya mtu
kutaka sifa pale mambo yanapokwenda vizuri, hata kama hukuchangia lolote
katika kuleta hali hiyo ya mafanikio. Yanapotokea matatizo, hulka ya
wengi ni kuruka kimanga na kusema sio wao.
Tunaweza kusema kwamba hakuna chombo
kilichoathiriwa na utamaduni huo hapa nchini kama Serikali. Mhimili huo
wa dola ndio umefanywa kama gunia la kufanyia mazoezi ya ndondi kwa
kugeuzwa kisingizio cha kila tatizo linalojitokeza. Hapana ubishi kwamba
yapo matatizo yanayosababishwa na mhimili huo.
Lakini, aghalabu mhimili huo umekuwa hautendewi
haki, kwani hata watendaji wake wanapohusika kufanya uamuzi fulani,
wanakuwa wa kwanza kuelekeza lawama kwa mhimili huo pindi uamuzi
walioufanya unatoa matokeo yasiyokubalika.
Mifano ni mingi, lakini kutokana na ufinyu wa
nafasi katika safu hii, tutatoa michache tu ya matukio ya hivi karibuni.
Hatua ya chama tawala (CCM), ambacho juzi kilitoa taarifa ya kuilaumu
Serikali kwa kuweka tozo ya Sh1,000 kwa kila laini ya simu ya kiganjani
imewaacha wananchi wengi wakiwa midomo wazi. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba chama hicho kilikuwa nyuma ya Serikali katika kufanya uamuzi wa
kuweka tozo hiyo. Baada ya tozo hiyo kupingwa na wananchi ndipo chama
hicho kilipoamua kuruka kimanga kwa malengo ya kisiasa.
Yafaa tukumbuke hapa kwamba tozo hiyo ilipitishwa
na Bunge katika kikao cha Bajeti mwezi uliopita wakati pia liliporidhia
Sheria ya Fedha. Serikali ilipeleka mapendekezo kuhusu tozo hiyo na
ilikuwa juu ya Bunge kuyakubali au kuyakataa. Zaidi ya theluthi mbili ya
wabunge wanatoka CCM na ukweli ni kwamba ndio haohao waliopitisha
Bajeti ya Serikali na mapendekezo yake kuhusu tozo ya laini za simu.
Hatua ya chama hicho kuilaumu Serikali baada ya tozo hiyo kupingwa na
wananchi ni kutoitendea haki katika kutaka kujinusuru kisiasa.
Utamaduni wa kutowajibika wakati matatizo
yanapotokea pia jana ulidhihirishwa na Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, Januari Makamba aliposema wizara yake haikubaliani na tozo
hizo. Inashangaza kuona viongozi wa wizara hiyo wanapingana na dhana ya
uwajibikaji wa pamoja, kwani tozo hiyo imewekwa na Serikali ambayo wao
ni watumishi wake. Ni mwendelezo wa utamaduni wa kuruka kimanga hata
kama nao walishiriki katika chombo kilichoamua kuanzisha tozo hiyo
inayopingwa na wananchi.
Ni utamaduni ambao sasa umejikita katika jamii
yetu. Undumilakuwili huo tunaoshuhudia katika suala la tozo ya laini za
simu ndio tulioshuhudia katika matukio mengi huko nyuma, likiwamo la
Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii ambayo ilipitishwa na Bunge kwa
msukumo wa idadi kubwa ya wabunge wa CCM, lakini wakaruka kimanga kwa
malengo ya kisiasa baada ya sheria hiyo kupingwa kila kona ya nchi. Ndio
maana tunasema katika hili la tozo ya laini za simu, Bunge ndilo libebe
lawama badala ya Serikali.
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment