TANGU kuanzishwa kwa vyama vingi nchini mwaka 1992, tayari chaguzi nne zinazoshirikisha vyama vingi zimefanyika.
Katika chaguzi hizo nne, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kushika dola kwa ushindi wa kishindo katika kiti cha urais, wabunge na madiwani.
Ushindi huu wa kishindo umeendelea kupungua kutoka ngazi ya ubunge na udiwani, ambapo wapinzani wamekuwa wakinyakua viti vya majimbo hata ambavyo vilikuwa vinatajwa kuwa ngome ya CCM.
Kupungua huko kwa viti vya ubunge na udiwani, ni kiashiria kuwa huenda kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi nchini, CCM itaenda katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, kikiwa hakina uhakika wa kushinda.
Wapinzani wakuu wa CCM ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kinashikilia rekodi ya pili kwa kuwa na viti vingi vya ubunge na udiwani nyuma ya CCM.
Nafasi ya ushindi katika uchaguzi huo, hasa katika ngazi ya urais imekumbwa na changamoto nyingi.
Wakati CCM imetimiza miaka 36 tangu kuzaliwa kwake, Chadema ina miaka 21 ambapo ndani ya miaka mitano kimeweza kujipambanua kwa Watanzania kama chama chenye sera madhubuti kinachotazamia kuchukua dola mwaka 2015.
Kwa nini CCM ikihofie Chadema na si vyama vingine? Ni mipango na mikakati ya muda mrefu, baada ya kuusoma mchezo wa CCM na kutumia udhaifu wake kujijenga.
CCM imewasahau wananchi wa kawaida na kukumbatia matajiri, Chadema ikaona hao ndio wanafaa na kuwafanya mtaji wao.
Ni ukweli ulio wazi kuwa mtaji wa chama chochote kile ni watu ambao ni wanachama hai.
Kitendo cha Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa wiki iliyopita mkoani Arusha, ni hatua kubwa waliyopiga ambayo imekifanya chama hicho kufikisha idadi ya viti 15 kwenye Baraza la Madiwani, wakati CCM kimebakiwa kuwa na viti 12.
Mbio za Chadema kuifukuzia dola kwa kusimama na miguu yake yenyewe katika uchaguzi mkuu wa tatu ulioshirikisha vyama vingi mwaka 2005, baada ya kuwa msindikizaji kwa mihula miwili ambapo ilimsimamisha Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wakati CCM ilimsimamisha Rais Jakaya Kikwete kwa mara ya kwanza.
Katika uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1995, Chadema ilishiriki uchaguzi huo bila ya kuweka mgombea urais, ambapo walikubaliana kumuunga mkono mgombea wa chama cha NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema ambaye alikuwa anakubalika sana wakati huo.
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Chadema ilishiriki tena uchaguzi huo kama mwanzo bila kusimamisha mgombea urais na safari hii ushirika ulihamia kwa CUF ambapo walimuunga mkono mgombea wake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mwaka huo, Chadema kilipata asilimia tatu ya kura za wabunge na jumla ya wabunge wanne na kushika nafasi ya nne katika vyama vya upinzani baada ya vyama vya CUF, TLP na UDP.
Baada ya kuchoka kuwa msindikizaji, Chadema ilijisuka upya na kumsimamisha Mbowe, ambaye alishindwa katika uchaguzi huo na hiyo ikawa kama changamoto kwa Chadema.
Chadema wakati huo ikaona ni wakati muafaka kujipambanua kwa wananchi, ambapo ilijieneza nchi nzima hata sehemu ambazo ilikuwa haikubaliki na kuvuna wanachama wengi zaidi.
Katika miaka yote hiyo CCM ilikuwa inaingia kwenye uchaguzi ikiwa na uhakika wa asilimia nyingi tu ya kushinda urais na viti vingi vya ubunge na udiwani bila kuhofia vyama vya upinzani.
Imani hii ya ushindi wa kishindo, inaanza kuyeyuka taratibu baada ya mwaka 2010, Chadema kupata viti vingi vya ubunge na udiwani hata katika majimbo ambayo yalikuwa ngome ya CCM.
Hofu ya kupoteza viti vingi vya ubunge na udiwani si hofu pekee inayoikabili CCM, bali pia inahofia kiti cha urais, haina uhakika nacho.
Tofauti kati ya Chadema na CCM baada ya uchaguzi ni kwamba, CCM hubweteka kwa madai ya kufanya kazi waliyotumwa na wananchi, lakini Chadema wao huchochea moto kwa kufanya mikutano mikoani yenye kauli mbiu za kuvutia kwa wananchi wanaopenda kusikia wanayotaka kusikia.
Mikutano hii imesaidia kuizindua CCM, ambapo nao hutembea mikoa iliyopitiwa na Chadema kujitakasa na kukanusha baadhi ya mambo baada ya jina lake kutiwa doa na Chadema.
Chadema imekuwa ikifanya mavuno katika vyuo vikuu mbalimbali pamoja na kuongeza idadi ya wanachama wanaotoka vyama vingine, wengi wao wakiwa viongozi.
CCM imekuwa ikifanya hivyo, lakini sasa ni kama imejisahau na inaanza upya ilipoishia.
Kujisahau huko kwa CCM kumeipaisha Chadema ambapo sasa ni vigumu kwa kijana wa kawaida kumueleza mambo hasi kuhusu Chadema.
Hii ni changamoto kwa CCM kushtuka na kuwakumbuka wananchi ambao kila uchao wanalalamikia ugumu wa maisha umeletwa na chama hicho.
Ni changamoto pia kwa Chadema kutobweteka kwa kuridhika na mafanikio madogo waliyo nayo.
No comments:
Post a Comment