Friday, March 14, 2014

Urusi:hatutaki vita na Ukraine


Urusi inaunga mkono mpango wa Crimea kupiga kura ya maoni kujiunga na Urusi
Balozi wa Urusi ndani ya Umoja wa Mataifa ameuambia mkutano wa dharura wa Baraza la usalama kuwa Moscow haitaki vita na Ukraine.
Vitaly Churkin alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Waziri mkuu wa mpito wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk.
Hata hivyo ametetea juu ya haki ya Crimea kupiga kura ya maoni kuhusu kujiunga na Urusi au la.
Ukraine imelalamika kuwa wahanga wa chokochoko za Urusi
Yatsenyuk ameliambia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa Moscow imekua ikikiuka Sheria na mikataba ya kimataifa, hata hivyo ana matumaini kuwa watakuwa na nafasi ya kuupatia suluhu mzozo uliopo kwa njia ya amani.
Kwingineko, mashariki mwa Ukraine mjini Donetsk, mtu mmoja ameuawa wakati wa vurugu za waandamanaji mahasimu, maofisa wameeleza.
Watu kadhaa pia wamejeruhiwa wakati mamia ya waandamanaji wanaoiunga mkono Urusi walipopambana na waandamanaji wanaoiunga mkono Kiev.
Machafuko haya yanaelezwa kuleta athari kubwa tangu kuanguka kwa Rais wa Ukraine Viktor Yanukovych, tarehe 22 mwezi Februari.
Kumekuwa na hali ya mvutano mkubwa wa kidiplomasia wakati kura ya maoni ikitarajiwa kupigwa na Raia wa Crimea.

No comments:

Post a Comment