Thursday, March 20, 2014

Bunge kurekebisha rasimu ya katiba TZ

 
Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuzindua rasmi shughuli za bunge la kitaifa kuhusu marekebisho ya katiba mjini Dodoma katika hatua itakayoanzisha rasmi mjadala wa kitaifa kuhusu marekebisho hayo.
Bunge hilo maalum la katiba limepewa kati ya siku 70 hadi 90 kujadili rasimu ya katiba na kisha kuifanyia marekebisho kabla ya kura ya maamuzi.
Kuna ripoti kwamba baadhi ya wajumbe kutoka upinzani na mashirika ya kiraia yanapanga kuvuruga shughuli hiyo ya uzinduzi.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa sehemu ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge kwa mujibu wa kanuni.
Mjadala huo uliwafanya baadhi ya wajumbe kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama ilivyokuwa imepangwa.
Kikao cha maridhiano kilifanyika siku hiyohiyo usiku na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu ndiposa Rais aweze kuzindua shughuli ya kujadili rasimu hiyo kabla ya kura ya maoni.

No comments:

Post a Comment