Saturday, March 1, 2014

Mtuhumiwa wa ugaidi akamatwa Uingereza

 
Moazzam Begg, mtuhumiwa wa ugaidi
Mfungwa wa zamani katika gereza la Guantanamo Bay,Moazzam Begg na mwananmke mmoja mwenye umri wa miaka 44 wamefunguliwa mashitaka yanayohusiana na makosa ya ugaidi nchini Syria.
Polisi wa West Midlands nchini Uingereza wamesema Bwana Begg, mwenye umri wa miaka 45, mkaazi wa Hall Green, Birmingham, ameshitakiwa kwa kutoa mafunzo ya kigaidi na kufadhili ugaidi nje.
Mwanamke anayeshitakiwa pamoja naye, Gerrie Tahari, wa Sparkbrook, Birmingham, anashitakiwa kwa kufadhili ugaidi nje ya nchi.
Watuhumiwa hawa watafikishwa mbele ya mahakama ya Westminster Jumamosi.
Watuhumiwa hao wawili walikamatwa Jumanne. Watu wengine wawili walikamatwa siku hiyo na kuwekwa mahabusu.
Watuhumiwa hao, mmoja mwenye umri wa miaka 36 anatoka eneo la Shirley, Solihull, na mwenye umri wa miaka 20 anatoka Sparkhill, Birmingham, ambao wanashikiliwa kwa tuhuma za kufadhili vitendo vya kigaidi nje.
Bwana Begg alikuwa akishikiliwa katika gereza la Marekani lililoko Guantanamo Bay nchini Cuba kwa karibu miaka mitatu.
Ni raia wa Uingereza ambaye alihamia Afghanistan pamoja na familia yake mwaka 2001, kabla ya kwenda tena Pakistan mwaka 2002 wakati vita vya Afghanistan vilipoanza.
Alikamatwa mjini Islamabad Januari 2002 na kupelekwa katika kituo cha Bagram nchini Afghanistan kwa karibu mwaka mmoja na baadaye kuhamishiwa Guantanamo.
Aliachiliwa mwezi Januari 2005 pamoja na raia wengine watatu wa Uingereza na kurejea Uingereza.
Bwana Begg, ambaye kwa sasa anaongoza kampeni ya kusaidia familia za watu wanaoshikiliwa magereza, hakuwahi kushitakiwa kwa kosa lolote.

No comments:

Post a Comment