Tuesday, July 9, 2013

‘POWER AFRICA’ YA OBAMA ITAFANYA TANESCO ISIONEKANE IPO ICU?

Rais Barack Obama wa Marekani.
NDUGU zangu tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuiona siku hii ya leo, hakika ni mwema kwetu.

Baada ya kusema hayo leo najadili kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwamba tangu lilipoanzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 1964 halijawahi kuwa na rekodi ya utendaji kazi wa kujivunia.

Hii hakuna anayebisha kwani kwa miaka 49, shirika hilo lingekuwa ni mtu tungesema limekuwa likiishi katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Mbaya zaidi ni kwamba shirika hili limekuwa likiugua huku ‘madaktari’ wake yaani wataalamu wanaoliongoza wengine wakiwa wamesomea nje ya nchi lakini wameshindwa kubaini ugonjwa.

Kwa miaka yote hiyo 49  hakuna mtu ambaye ameweza…

Rais Barack Obama wa Marekani.
NDUGU zangu tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuiona siku hii ya leo, hakika ni mwema kwetu.
Baada ya kusema hayo leo najadili kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwamba tangu lilipoanzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 1964 halijawahi kuwa na rekodi ya utendaji kazi wa kujivunia.
Hii hakuna anayebisha kwani kwa miaka 49, shirika hilo lingekuwa ni mtu tungesema limekuwa likiishi katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Mbaya zaidi ni kwamba shirika hili limekuwa likiugua huku ‘madaktari’ wake yaani wataalamu wanaoliongoza wengine wakiwa wamesomea nje ya nchi lakini wameshindwa kubaini ugonjwa.
Kwa miaka yote hiyo 49  hakuna mtu ambaye ameweza kutegua kitendawili kuhusu faida inayopata serikali yenye asilimia 100 ya umiliki kwa kuendelea kulikumbatia shirika hilo na matokeo yake ni wananchi kuumia kwa tozo kubwa ya umeme.
Mwaka jana walipoteuliwa mawaziri wapya kuiongoza Wizara ya Nishati na Madini, wananchi wengi walipata matumaini makubwa, kwani Waziri Dk. Sospeter Muhongo na naibu wake George Simbachawene walionyesha ari kubwa ya kulibadilisha shirika hilo lililokuwa limeoza kutokana na vitendo vinavyodaiwa kuwa ni vya rushwa na ufisadi, kuwa shirika lenye ufanisi likiwa na watumishi wachapakazi wenye ari na uadilifu wa hali ya juu.
Ajabu ni kwamba shirika limeanza tena mbinu chafu za kujihujumu lenyewe kwa kushindwa kusambaza umeme kwa visingizio visivyokuwa na vichwa wala miguu. Nimepata malalamiko ya watu lukuki wakilalamikia kucheleweshewa kupatiwa umeme sehemu mbalimbali nchini.
Rais Barack Obama wa Marekani wiki iliyopita alipotembelea Tanzania alitoa ahadi lukuki lakini ambayo imewafurahisha wengi ni ya kuboresha umeme nchini mwetu na nyingine saba katika Afrika.
Alitangaza mpango wa uzalishaji wa umeme wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 7 katika nchi hizo licha ya kuwa na  mpango wa kukinga ukimwi wenye thamani ya dola bilioni 4.2 pamoja na msaada unaolenga kuimarisha usalama wa chakula wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 140.
Kubwa ambalo ni dhahiri ni kwamba Rais Obama, alisema  Afrika itajengwa na Waafrika wenyewe na kwamba nchi kubwa kama Marekani inasaidia kuchochea maendeleo na kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.
“Hatutaki kusambaza umeme bali tunafanyakazi kwa karibu na serikali pamoja na wadau muhimu kuangalia sheria na miongozo itakayosaidia sekta binafsi kuwekeza zaidi...,” alisema Obama wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari Ikulu Dar.
 Alisema Tanzania pia itanufaika na mpango wa Marekani wa ‘Power Africa’ ambao umetengewa dola bilioni saba kwa ajili ya kuufanikisha. Obama hakumung’unya maneno alisema lengo ni kuibua fursa za uwekezaji na biashara kwa kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana kwa ajili ya kuendesha viwanda.
Lililowafurahisha watu ni pale aliposema kuwa mkakati huo  unalenga kuwapatia Watanzania na Waafrika umeme wa uhakika na kwa bei nafuu na wananchi walifurahi kutokana na nishati hiyo kuwa ghali sana katika nchi yetu.
Ndugu zangu, wananchi wamelalamika sana kuhusiana na bei ya umeme nchini lakini kilio chao kimekuwa kama cha samaki katika maji, machozi hayaonekani! Obama baada ya kuja nchini alikwenda kutembelea mitambo ya Kampuni ya Symbion. Hii ni mitambo ambayo miaka 4 iliyopita ilipigiwa kelele bungeni kuwa ni chakavu, Tanesco wakakatazwa kuinunua badala yake kampuni hiyo ya Kimarekani ikainunua, wakaingia  mkataba na Tanesco kuwauzia umeme unaozalishwa na mitambo hiyohiyo iliyokejeliwa.
 Wakati tunasuburi kulipa takriban shilingi 105 bilioni kwa Dowans baada ya kutubwaga kwenye kesi, tulishuhudia Obama akienda katika mitambo ile ‘chakavu’ na viongozi wa serikali yetu! Sisi watu wa kawaida tunajiuliza tena kimoyomoyo,’Si walisema mitambo hii ni chakavu?’
Naamini bado kitambo kidogo suala la nchi kuingiza gizani itakuwa ni historia kwani tumeambiwa kampuni kubwa ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme ya GE imetangaza kuingia ubia na Kampuni ya Symbion kuzalisha umeme nchini na takriban 400MW zitazalishwa kutoka Mtwara na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Nishati naona ni kipaumbele kikubwa sana kwenye ziara aliyoifanya Obama nchini. Kwa nchi kama yetu yenye watu asilimia 21 tu wenye umeme, ni dhahiri kipaumbele hiki kimeungwa mkono. Hata hivyo, Obama ni lazima asimame kidete kuhakikisha kuwa kampuni za nchini mwake zinazopata mikataba hapa nchini ziweke wazi mikataba hiyo na kulipa kodi inavyostahili.
Uwazi wa mikataba na uwezo wa kupambana na ukwepaji kodi ni muhimu sana katika vita dhidi ya ufisadi na ubadhirifu, uzalishaji ukianza mapato yao na kilicholipwa kwa serikali ni vema viwe vinawekwa wazi na hilo naomba Obama mwenyewe ayasisitize makampuni ya nchini mwake yanayokuja kuwekeza hapa kwetu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment