Tuesday, July 9, 2013

KIKWETE MSHANGAO


Rais Dk. Jakaya Kikwete akihutubia katika Tamasha la Matumaini 2013.
Na Waandishi Wetu

TAMASHA la Matumaini mwaka 2013 limefanyika juzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete kulihutubia taifa kupitia tamasha hilo huku akionesha kushangazwa jinsi maandalizi yake yalivyofanyika.…

Rais Dk. Jakaya Kikwete akihutubia katika Tamasha la Matumaini 2013.
Na Waandishi Wetu
TAMASHA la Matumaini mwaka 2013 limefanyika juzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete kulihutubia taifa kupitia tamasha hilo huku akionesha kushangazwa jinsi maandalizi yake yalivyofanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo akitoa neno katika tamasha hilo.
Akizungumza moja kwa moja ‘laivu’ kwa Runinga ya Taifa (TBC1) iliyoweka kamera zake kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema tamasha hilo ni zuri sana kwa sababu linawakutanisha Watanzania wenye itikadi mbalimbali na kuwafanya kuwa kitu kimoja.
AIMWAGIA SIFA GLOBAL PUBLISHERS
JK aliipongeza Kampuni ya Global Publishers inayochapa Magazeti ya Uwazi, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani, Ijumaa na Championi kwa kufanikisha tamasha hilo lenye mvuto.

Rais JK akimpongeza Shigongo.
AMPA TANO ERIC SHIGONGO
Akiendelea kuhutubia Watanzania, Rais Kikwete alikwenda mbele zaidi kwa kumpongeza binafsi Mkurugenzi wa Global Publishers, Eric Shigongo kwa kuwa kinara wa kubuni tamasha hilo.  

AWATUMA WABONGO, AWATAKA  WASIMUNG’UNYE  MANENO
Katika hatua nyingine, rais alitumia nafasi hiyo kuwaambia Watanzania kuwa waende wakawaambie wanasiasa wanaopenda kusababisha machafuko katika jamii kuwa wanachokifanya siyo kwani wanahatarisha amani na umoja uliopo. Rais alisema: “Tena mkawaambie bila kumung’unya maneno.”

AMTAJA MBUNGE JOSHUA NASARI WA CHADEMA
Katika hali ambayo wengi hawakuitarajia, mheshimiwa rais alisema Tamasha la Matumaini limeweza kuwakutanisha wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala (CCM).
JK: “Mfano, tamasha hili limewakutanisha Mheshimiwa Joshua Nasari (Arumeru Mashariki-Chadema) na Mheshimiwa William Ngeleja (Sengerema-CCM)…”
Kauli hiyo iliamsha msisimko kwa watu waliohudhuria tamasha hilo huku wengi wakisema JK ni rais asiyekuwa na kinyongo na mpinzani yeyote.
“Umeona, mshikaji (rais) hana kinyongo na mpinzani yeyote, analitaja jina la Nasari kama ni mbunge wa CCM, angekuwa rais mwingine asingelitaja jina la mpinzani,” alisema shabiki mmoja wa timu ya Wabunge wa Yanga.

Rais JK akihesabu wachezaji kabla ya kuanzisha mechi.
MSHANGAO WA WABONGO KWA JK
Zamu ikafika ya JK kuwashangaza Wabongo waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa siku hiyo. Mshangao huo ulitokea wakati mheshimiwa rais aliposhuka jukwaani kwenda uwanjani kwa lengo la kukagua timu zote na pia kupuliza kipyenga cha kwanza kuashiria kuanza kwa mpira.
JK, alikuwa ameongozana na wana usalama wake, sanjari na Bosi wa Global, Shigongo na wapiga picha kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya ndani ya nchi.
Baada ya kukagua timu, ratiba ilimuonesha kuwa alitakiwa kusimama dimbani na kupuliza kipyenga cha kuashiria kuanza kwa kandanda.
Hata hivyo, rais aliangalia pande zote na kugundua kuwa mapaparazi walikuwa karibu naye ndani ya uwanja huo kitendo ambacho kingemfanya ashindwe kuanzisha mpira.
Ikabidi aseme: “Wapiga picha ondokeni nichezeshe mpira.”
Kauli hiyo iliwachekesha wengi huku wakiwa wameshangaa. Baadhi ya watu walisikika wakisema kuwa JK aliitoa kauli hiyo kama refa tu na si rais, wakampongeza kwa kusema kauli yake ilionesha umoja katika siku kama hiyo bila kujali nafasi yake katika taifa.
Wapiga picha waliitii kauli ya mheshimiwa rais, walitoka nje ya alama ya mwisho ya uwanja na kumpa nafasi JK apulize filimbi iliyosikika uwanja mzima na watu kushangilia kisha akampa filimbi refa wa mchezo huo, Othman Kazi.

WABUNGE WAELEZA YA MOYONI 
Uwazi lilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano walioshiriki katika mpambano wa Simba na Yanga.

IDD AZZAN, CCM-KINONDONI
“Aah! Kwa kweli mpambano ulikuwa mkali, ilifika mahali nilihisi kuchoka zaidi, lakini mazoezi ya nguvu ninayofanya kila siku asubuhi yalinisaidia sana nikamaliza dakika zote sabini nikiwa fiti.”

AMOS MAKALLA, CCM- MVOMERO
“Ukiniangalia hivi si unaweza kusema siwezi kuruka dimbani, lakini vipi mlionaje mashuti yangu uwanjani? Sema tu bahati haikuwa yetu Simba.”

 JK akisalimiana na Halima Mdee wa Yanga.
HALIMA MDEE, CHADEMA- KAWE
“Tena Simba washukuru mimi sikupangwa, ningewapiga mabao bila kufikia hatua ya matuta (penati). Wana bahati sana.”
Katika mpambano huo, Wabunge wa Yanga waliwalaza wenzao wa Simba kwa matuta 4-3.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Ngoyai Lowassa.
LOWASSA NAYE ATOA NENO LAKE LA MOYONI
Naye Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM, Edward Ngoyai Lowassa alisema alitamani sana kuwepo kwenye tamasha hilo.
Akizungumza na Uwazi kwa njia ya simu juzi, Mheshimiwa Lowassa alisema yuko Mwanza kwa shughuli za kikazi, lakini kama angekuwepo jijini Dar angehudhuria Tamasha la Matumaini ambalo alisema limeukonga moyo wake.

Waziri wa Habari,  Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt Fenella Mukangara wakati akimkaribisha JK kutoa hotuba yake.
WAZIRI MUKANGARA AWA KIVUTIO KWA MSUKO WA NYWELE WA TWENDE KILIONI
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara  alikuwa kivutio kwa watazamaji wanaomfahamu kupitia vyombo vya habari kufuatia kutinga uwanjani akiwa na ule msuko wake wa nywele maarufu kwa jina la Twende Kilioni.
Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la mama Hamida alisema: “Toka nimeanza kumwona Waziri Mukangara mwaka juzi sijawahi kukuta kichwani kitu tofauti na Twende Kilioni, nadhani ameamua kuwa ndiyo mtindo rasmi wa nywele zake.”

SHIGONGO AWASHUKURU WATANZANIA
Akizungumza na Uwazi uwanjani hapo baada ya tamasha kumalizika, Shigongo alisema anawashukuru sana Watanzania wote kwa jinsi walivyoitikia wito wa kufika kwa wingi uwanjani.
Alisema Tamasha la Matumaini ni la kila mwaka na lengo lake kuu ni kuwakutanisha Watanzania katika umoja wenye kuondoa tofauti za kiitikadi na kidini ili Tanzania iendelee kuwa na amani na mshikamano ulioachwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Asante yangu ni kwa Watanzania wote waliofika leo hapa Uwanja wa Taifa, kwa kweli nimefurahi sana. Tamasha hili ni la kila mwaka, lengo ni kuondoa tafauti za kiitikadi na kidini, nchi yetu iendelee kuwa na mshikamano ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere,” alisema Shigongo

No comments:

Post a Comment