Monday, February 24, 2014

Ligi Kuu England yazidi kupamba moto


 
Wachezaji wa Arsenal wakipongezana kwa ushindi katika moja ya mechi zao za ligi kuu England
Ligi kuu ya England iliendelea mwishoni mwa wiki, ambapo vigogo wa ligi hiyo waliendelea kujiimarisha katika nafasi zao kwa kupata matokeo mazuri.
Mchezo wa Jumapili kati ya Liverpool dhidi ya Swansea, ulimalizika kwa Liverpool kushinda magoli 4-3. Jordan Henderson na Daniel Sturridge wa Liverpool waliifungia timu yao magoli mawili mawili kila mmoja katika mchezo uliojaa ushindani mkubwa.
Matokeo mengine ni Newcastle kuilaza Aston Villa goli 1-0, huku nayo Norwich ikiiduaza Tottenham goli 1-0.
Michezo ya Jumamosi ilizikutanisha Arsenal na Sunderland. Arsenal ilitoa kipigo cha hasira kwa kuibamiza Sunderland magoli 4-1, ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu ya England baada ya kufungwa na Bayern Munich ya Ujerumani magoli 2-0 katika michezo ya UEFA.
Eden Hazard wa Chelsea
Chelsea ilipata ushindi wa dakika za majeruhi dhidi ya Everton kwa kuifunga bao1-0, huku Mancity nayo ikipata ushindi mwembamba kwa uilaza Stoke bao 1-0. Nayo Manchester United inayochechemea katika ligi hiyo, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace.
Kwa matokeo hayo, Chelsea iliyocheza mechi 27 inaongoza kwa pointi 60, huku ikifuatiwa na Arsenal yenye pointi 59 baada ya kucheza pia michezo 27. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Machester City yenye pointi 57 ikiwa imecheza michezo 26. Liverpool imejikusanyia pointi 56 baada ya michezo 27, ikiwa katika nafasi ya nne.
Manchester United imejikongoja na kushika nafasi ya sita baada ya kupata pointi 45 sawa na Everton, lakini Everton ikiwa na mchezo mmoja zaidi.
Mpaka sasa Fulham ndiyo inayoshikilia mkia kwa kuwa na pointi 21 katika michezo 27 iliyocheza. Juu yake ni Cardiff yenye pointi 22 na Sunderland ina pointi 24. Timu hizo ziko katika hatari zaidi ya kushuka daraja.

No comments:

Post a Comment