Friday, February 28, 2014

Kilwa Kutumia Rasilimali Kuboresha Maisha ya Wananchi


Ramani ya hospitali ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa itakayojengwa wilayani Kilwa kwa nguvu za halmashauri na wadau wa Maendeleo.
Ramani ya hospitali ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa itakayojengwa wilayani Kilwa kwa nguvu za halmashauri na wadau wa Maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Adoh Mapunda (katikati) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu namna wilaya hiyo inavyoendelea kuboresha huduma za jamii kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizo katika wilaya hiyo. Kushoto ni diwani wa kata ya Kikole Mwl. Haji Mulike na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Ali Mohamed Mtopa. Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Adoh Mapunda (katikati) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu namna wilaya hiyo inavyoendelea kuboresha huduma za jamii kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizo katika wilaya hiyo. Kushoto ni diwani wa kata ya Kikole Mwl. Haji Mulike na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Ali Mohamed Mtopa. Picha zote na Aron Msigwa – MAELEZO

Na Aron Msigwa – Maelezo, Dar es Salaam UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa umesema utahakikisha rasilimali zote zinazopatikana katika wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na gesi asilia zinatumika kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Adoh Mapunda wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizo katika wilaya hiyo.
Akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, watendaji na baadhi ya Madiwani wanaohudhuria kikao kazi jijini Dar es Salaam, Mapunda alisema kuwa halmashauri hiyo imejipanga kupunguza utegemezi wa fedha toka serikali kuu kwa kupanua wigo wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Amevitaja vyanzo hivyo vipya ni pamoja na ushuru wa zao la Ufuta ambalo sasa mapato yake yamefikia milioni 595, mauzo ya viwanja na ushuru wa Gesi asilia inayozalishwa katika Kijiji cha Songosongo ambayo sasa inatoa asilimia 0.3 ikiwa ni ushuru wa tozo la huduma.
Akifafanua kuhusu mapato hayo, Mapunda alisema kuwa katika zao la ufuta asilimia 20 ya pato hilo inarudishwa vijijini na halmashauri hiyo na kuongeza kuwa mapato ya ushuru wa huduma unaolipwa kwa halmashauri kutokana na shughuli za gesi za kampuni ya PAN AFRICAN ENERGY katika eneo la Songosongo huchangia 20% kwa ajili ya maendeleo ya eneo hilo.
“Kuanzia mwezi Septemba 2012 Baraza la Madiwani lilipendekeza tuanze kupeleka asilimia 20 kwenye kijiji cha Songosongo kutokana na malipo ya kampuni ya PAN AFRICAN ENERGY kiasi cha shilingi milioni 811ambapo hadi sasa tumeshapeleka jumla ya shilingi milioni 139 na tunajiandaa kupeleka kiasi kingine kilichobaki cha shilingi 22,” alisema Mapunda.

Akitoa ufafanuzi kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii mkurugenzi huyo alisema Wilaya ya Kilwa inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya Maji Safi, Umeme, Elimu, mkakati wa kukuza ajira, kuimarisha ulinzi na usalama kwa kujenga kituo cha polisi cha kisasa kitakachogharimu shilingi milioni 625 na uboreshaji wa huduma za afya.

Aliongeza kuwa katika kuboresha huduma za afya wilaya hiyo imeshatenga eneo la hekari 30 kwa ajili ujenzi wa hospitali ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa itakayotoa huduma ya afya kwa wakazi wa wilaya hiyo.

“Mradi huu wa hospitali ya kisasa utaanza haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka huu hii ikiwa ni mchango wa rasilimali za eneo letu pia kwa kushirikiana na kampuni inayochimba gesi, pia tunajiandaa kwa ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa kimataifa utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8,” alifafanua.

Aidha katika hatua nyingine, Mapunda ameeleza kuwa halmashauri ya Kilwa inaendelea na mikakati ya kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuimarisha usafiri wa ndani wa wilaya hiyo, kufanya juhudi ya ukamilishaji wa miundombinu ya ulinzi na usalama ili kuimarisha hali ya ulinzi na usalama wa miundombinu iliyopo.

No comments:

Post a Comment