Friday, March 14, 2014

Rwanda na Afrika.K zalipizana kisasi

 
Luteni Generali Kayumba Nyamwasa
Serikali ya Rwanda imesema hatua ya kuwatimua maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ni ya haki na ilizingatia uchokozi ambao ulianzishwa na serikali ya Afrika Kusini yenyewe kwa kufukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Rwanda.
Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ,Bi Louise Mushikiwabo, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter ameeleza kwamba Rwanda ilikuwa na haki zote kuwafukuza mabalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ikizingatia hatua ambayo nchi hiyo ilianzisha yenyewe kwa kuwatimua maafisa wa ubalozi wa Rwanda mjini Johannesburg.
Katika ujumbe wake mfupi kwenye mtandao huo Bi Mushikiwabo, anailaumu Serikali ya Afrika Kusini kwa kutochukua hatua dhidi ya wanyarwanda waliokimbilia nchini humo ambao serikali ya Rwanda inawatuhumu kuendelea na hujuma za kigaidi dhidi ya Rwanda na kwamba Pretoria haijatekeleza muafaka uliofikiwa awali.
Kulingana na kiongozi huyo kupitia mtandao wa twitter, mahusiano mema kati ya Rwanda na Afrika Kusini yatafikiwa wakati suala la kisheria kuhusu wanyarwanda waliokimbilia nchini humo itapata ufumbuzi.
Wakati haya yakiarifiwa ,mjumbe maalum wa Rais Baracka Obama wa Marekani katika mataifa ya ukanda wa maziwa makuu, Russ Feingold,alisema kuwa Marekani inafuatilia kwa karibu mzozo huo ambao alielezea waandishi kwamba mataifa ya Rwanda na Afrika ya kusini hayana budi kumaliza tofauti zao kwa njia ya kidiplomasia.
Mjumbe huyo alikutana na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukutana na Rais Paul Kagame.
Miongoni mwa wanyarwanda waliokimbilia Afrika ya kusini ni Generali Kayumba Nyamwasa ambaye amekuwa akilaumu utawala wa Rwanda kwa kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi yake ambayo amenusurika.
Kwa upande mwingine Serikali ya Rwanda inakanusha vikali kuhusika na tuhuma hizo.
Kayumba Nyamwasa anajulikana kama mtu aliyetangaza wazi kupiga vita utawala wa Rwanda na anatuhumiwa kuhusika katika mashambulizi ya hapa na pale yanayogharimu maisha ya watu na mali.

No comments:

Post a Comment