Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
AMA kweli duniani kuna mambo kwani dereva na abiria wa basi la
Manchester ambalo namba yake haikujulikana mara moja, lililokua likitoka
Lindi kwenda jijini Dar es Salaam walijikuta wakiangua vilio baada ya
kumuona mwenzao akijichinja hadi kufa kwa kisu ndani ya gari hilo.
Kwa mujibu wa chanzo, tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa tisa
alasiri, Jumatano wiki iliyopita mara basi hilo lilipofika katika hoteli
moja ya Nangulukulu kwa ajili ya kupatia chakula.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari hii jijini
Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya abiria
walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa mara walipofika katika hoteli
hiyo, kila mmoja alitawanyika kwa lengo la kujipatia chakula na baadhi
yao walienda maliwatoni akiwemo marehemu huyo.
Walisema kwamba marehemu huyo ambaye jina lake halikupatikana mara
moja, wakati wa kushuka hakuonekana na kisu aina ya sime lakini baadaye
abiria wachache waliotangulia kwenye gari, walimshuhudia akiwa ameshika
sime hiyo mkono pasipokujua aliipata wapi.
“Hata sisi tulishangaa kumuona akiwa karibu na usukani wa dereva
huku akizamisha sime tumboni kisha kuichomoa na kujichinja shingoni
hadi pale alipokuwa akivuta koromeo na kuning’inia.
“Tulichanaganyikiwa kwani ni kitu ambacho hatukukitarajia na wala
hatujawahi kushuhudia tukio kama hilo la mtu kujichinja hadharani,
tulibakia kutokwa machozi huku akina mama wakipiga yowe, hakuna mtu
aliyethubutu kumsogelea kumuokoa kwani kila mmoja alimuogopa.
“Tulishindwa kupanda basi hilo kwani ni tukio la ajabu pia ndani kwa
mbele kulikuwa kumetapakaa damu, ghafla alidondoka chini ndani ya gari,
aliomba kalamu na karatasi ili kuandika ujumbe.
“Dereva alichukua kalamu na kipande cha karatasi na kumpa, alianza
kuandika huku damu ikimbubujika tumboni na shingoni, hatukujua
alichokiandika, aliishiwa nguvu taratibu akadondoka.
“Abiria walimsogelea na kumuinua na walimueleza kuwa atubu kwa Mungu
kosa alilolifanya kabla hajafa, alipiga magoti na kuomba, ghafla
alidondoka tena.
“Kaka yake ambaye alikuwa akisafiri naye kuelekea Dar es Salaam
alichanganyikiwa kwani hakutegemea kuwa mdogo wake angejiua, kwani
alisema hana historia ya kuugua ugonjwa wa akili. Polisi walipigiwa simu
na walifika kumchukua lakini baada ya muda mfupi akawa amefariki dunia.
“Sisi abiria wengine tuliendelea na safari kuelekea Dar es Salaam ambapo marehemu na kaka yake walibakia huko mkoani Lindi.
“Mara tulipofika Dar es Salaam dereva alitusihi tukae kimya kwa
dakika moja na kuomba kutokana na tukio lililotupata, tulifanya hivyo
baadaye kila mmoja alitawanyika na kuelekea kwake,” kilisema chanzo kwa
sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Renatha Mzinga alipoulizwa
mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusiana na tukio hilo alikiri kutokea.
“Ni kweli tukio hilo lilitokea lakini kwa sasa sina data kwani nipo
njiani nikitokea Nairobi, Kenya kikazi kuelekea Lindi, mara nitakapofika
huko ofisini ndipo nitapata tukio zima lilivyokuwa,” alisema Kamanda
Mzinga.
No comments:
Post a Comment