MWENYEKITI wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho amekiri kuwasilisha waraka kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba na kupendekeza Zanzibar na Tanganyika kuwa na mamlaka huru, hatua ambayo imezua malalamiko miongoni mwa makada wa chama hicho ambao wamesema huo ni usaliti.
Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma, Kificho ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), alisema kimsingi waraka huo ulilenga kuipa nguvu Zanzibar kushughulikia mambo yasiyo ya Muungano ili kujiimarisha kiuchumi.
Kauli ya Kificho inakuja wakati baadhi ya wajumbe wa CCM kutoka Zanzibar wakiitisha mkutano na kutoa tamko la kumshutumu kwa kutoa mapendekezo hayo, wakisema ni kinyume na msimamo wa chama hicho. Kificho alionyesha kushangazwa na madai kuwa mapendekezo hayo yaliyoandaliwa na watu wanne ambayo ameyasaini si msimamo wa BLW.
“Tatizo lililopo ni tafsiri ya kila mmoja anapousoma waraka huo, hakuna sehemu tuliyoandika tunataka Serikali tatu, mamlaka huru maana yake kila upande uwe na uwezo wa kushughulikia mambo yake yasiyo ya Muungano na kujijenga kiuchumi, ikiwa ni pamoja Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya Kimataifa (OIC) na siyo kuunda dola,” alifafanua Spika Kificho.
Alisisitiza kuwa angependa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano yaendeshwe na Zanzibar bila ya kuwekewa vikwazo mahali popote. Madai hayo ni dalili za wazi za mgawanyiko baina ya wajumbe wa CCM ambao wameanza kuonyesha makundi mawili yenye misimamo tofauti.
Kundi linalomshutumu Kificho, linawajumuisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Juma Ali Shamhuna, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Spika wa BWZ, Ali Abdallah Ali.
Jana, kundi hilo lilimtuhumu Kificho kuwa hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo Serikali tatu aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Hata hivyo, mtazamo huo wa BLW unatofautiana na ule wa Kificho uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, ukipendekeza Serikali tatu.
“Kwa vile mfumo wa Serikali mbili uliopo sasa hauwezi kujenga Muungano utakaohimili mabadiliko ya kisiasa na kwa vile umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa umeshindwa kujenga Muungano imara, uachwe katika kuendesha Muungano wa Tanzania,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Othman.
Jana asubuhi, zaidi ya wajumbe 10 wa Baraza la Wawakilishi akiwamo Shamhuna, Nahodha na Ali waliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma na kumtupia lawama Kificho wakisema; “Amewasaliti katika mchakato huo wa Katiba.”
Akizungumza katika mkutano huo, Mnadhimu wa BWZ ambaye pia ni Katibu wa Wawakilishi wa CCM, Salmin Awadh Salmin alisema katika uwasilishaji wa maoni ya taasisi hiyo katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Baraza la Wawakilishi halikutumia fursa hiyo ipasavyo.
“Ni viongozi wachache tu waliobeba jukumu hili kubwa na zito bila kuwashirikisha wajumbe walio wengi. Sisi wawakilishi tunashukuru kwa taasisi yetu hii kupatiwa heshima kubwa ya kutoa maoni yetu ingawa utekelezaji wake haukuendana na malengo tuliyokusudia.
“…Ieleweke kwamba sisi Wawakilishi wa CCM hatukuwa sehemu ya maoni yaliyowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa vile jambo hilo lilifanyika kwa siri bila kutolewa taarifa kwa viongozi wakiwamo viongozi wa Kamati ya Uongozi.”
Alisema ni jambo la ajabu na kushangaza kuona taasisi kubwa kama Baraza la Wawakilishi, kuteleza kwa kiasi hicho.
“Tulitarajia baada ya kuteleza huko tungepatiwa taarifa ili kutambua kilichotendeka. Taarifa na maoni hayo yaliyotolewa kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi hayakuwa na baraka wala kuvihusisha vikao husika,hivyo kubeba zaidi maoni binafsi ya viongozi waliohusika,” alisema na kuongeza:
“Tunaendelea kusisitiza kwamba hatukuwahi kukutana wala kuamua kuwasilisha maoni hayo, tunatambua pengine wenzetu hao walikuwa na dhamira njema na pana zaidi hadi kusababisha utaratibu kusahaulika.”
“Tunapenda kutumia nafasi hii kuwatoa hofu viongozi na wanachama wetu kwamba Wawakilishi wa CCM katu hatutakisaliti chama chetu na wanachama wake.
Tutasimamia maelekezo na miongozo ya CCM kwa gharama yoyote huku tukiamini kwamba Muungano imara na endelevu ni wa Serikali mbili.”
“Document (waraka), iliyotolewa ameisaini mwenyewe na jana (juzi) tulivyozungumza (Kificho) alikubali kuwa ni document sahihi na ni document aliyoisoma wakati akiwasilisha hiyo taarifa. Kwa hiyo mmoja ni yeye (Kificho), ambaye aliwasilisha mwenyewe, wengine pengine anawafahamu mwenyewe, lakini sisi hatuwafahamu.”
Alipoulizwa walikuwa wapi tangu Jaji Warioba alipotoa msimamo wa Baraza la Wawakilishi, Salmin alijibu: “Ni muda mrefu na wakati Jaji Warioba alipowasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa msimamo wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni Serikali tatu, sisi tulishangazwa sana kauli hiyo.
“Mimi mwenyewe nikiwa Mnadhimu niliwasiliana na kiongozi wa taasisi ile (Kificho), nikamuuliza kuhusu taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akanihakikishia kuwa taarifa hiyo siyo sahihi na sivyo ilivyokuwa.”
No comments:
Post a Comment