Nianze
kwa kuwapa ‘hi’ madenti wote Tanzania nzima, anko wenu nipo katika
Viwanja vya Bunge mjini Dodoma kama mmoja wa mashahidi wa nini wale
wawakilishi wa makundi mbalimbali ambayo Rais Jakaya Kikwete aliwateua
kujumuika pamoja kupitia rasimu ya katiba ili waweze kutengeneza katiba
mpya ambayo huenda ni watoto wenu nyinyi au wajukuu zangu mimi, watakaa
tena miaka 50 ijayo kuirekebisha kulingana na mazingira ya wakati huo.
Ni jambo zito sana, ingawa najua kabisa ni wachache sana kati yenu
ambao mnafuatilia na kwa jinsi mnavyoishi, mimi hata sishangai. Ni
rahisi nyinyi kujua kibao gani kipya Rihanna katoa, Jay Z kasema nini au
Beyonce kafanya tukio gani lililovunja rekodi.
Labda niwaambie kitu kimoja. Hapa Dom, ambako ni Makao Makuu ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndipo niliposoma sekondari
na kidogo shule ya msingi. Ninapajua kama kiganja changu. Naijua mitaa
balaa, ingawa hiyo ni miaka 20 iliyopita.
Kama nilivyosema mwanzo, zaidi ya Watanzania 600 wapo hapa kujadili
rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Tume Maalum ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye miaka ya nyuma, nyinyi
mkiwa wadogo na baadhi yenu hamjazaliwa, alipata kuwa Waziri Mkuu na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Yeye alikuwa mwenyekiti na makamu wa tume hiyo ambayo iliundwa na
Rais Jakaya Kikwete. Lakini pia ndani ya tume hiyo, walikuwepo viongozi
wengi wa enzi zetu sisi, walioheshimika sana, akiwemo katibu mkuu wa
zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, enzi hizo ikijulikana kama OAU,
Dk. Salim Ahmed Salim.
Hawa watu walizunguka nchi nzima, kuwasikiliza wananchi wa aina na
rika zote, nini wanadhani wanaona kinafaa kuwa ndani ya katiba yetu.
Labda niwaulize, mnajua katiba ni nini? Najua wengi wenu hamjui, labda
kama ‘Diamond Platinumz’ ataamua kuiweka katika moja ya vibao vyake,
labda mtaijua.
Katiba ni sheria mama ya nchi, ndani yake haki ya kila mtu, kila
kada, kila jamii imetafsiriwa. Sheria zote, zile za polisi, ardhi,
misitu, mahakama na kila aina ya sheria utakayoambiwa, msingi wake
mkubwa ni ndani ya katiba. Hakuna sheria wala kanuni yoyote
itakayokubana wewe kama haipo ndani ya katiba hii ambayo inajadiliwa,
kukubaliwa na hatimaye kutiwa saini kama sheria na wenzetu hawa wapatao
600!
Hili ni jambo kubwa sana ambalo kwa makusudi, tumekataa
kulitambua uzito wake badala yake bado tunapigiana simu, kutumiana SMS,
kuchati katika Facebook na Twitter kuelezana wapi leo tutakutana, wapi
kuna tamasha na nani atatumbuiza!
Tukio hili ni la kihistoria, halijawahi kutokea katika nchi yetu
tokea ipate uhuru mwaka 1961! Hata hao wanasiasa wakubwa mnaowasikia,
hawajawahi kushuhudia utayarishwaji wa katiba mpya ya nchi yetu. Wote
kwa ujumla wetu, hii ni mara ya kwanza ambayo ninaamini kabisa, kama
ikienda sawa, mimi anko wenu sitashuhudia tena Watanzania wakikaa na
kujadili katiba mpya!
Unajua kwa nini sitashuhudia? Hiyo labda itatokea miaka 50 ijayo.
Unadhani nitakuwepo kwa maisha haya ya chipsi kuku, juisi za magumashi
za Buguruni na viroba? Thubutu!
Ninachotaka kuwaambia sasa, hili jambo siyo la wale jamaa wanaosema
posho ya shilingi laki tatu kwa siku haiwatoshi, hili ni jambo lenu
nyinyi maanko kwa sababu vile vibabu pale vinawaandalia mustakabali wa
maisha yenu kama taifa hapo baadaye.
Ni lazima mfuatilie kwa umakini mkubwa kinachoendelea hapa Dodoma,
mjue wanawapa nini, kwa sababu baadhi yao, ambao mimi ninawapinga, eti
wanataka katiba ya kulinda maisha yao ambayo imebaki miaka mitano au
kumi ijayo!
Fuatilieni, hasa nyinyi ambao mpo vyuoni na hata sekondari, msikubali
wawape katiba ambayo kumbe baadaye mtagundua kuwa inawalinda watoto
wao, vimada wao na hata mashemeji zao. Bado hamjachelewa, mkiona
wanawazingua niiteni, niambieni na mimi kwa kushirikiana na wapambanaji
wenzangu, tutawapa za chembe!
Niwaage kwa kuwaambia kuwa maisha ya Dodoma wala siyo magumu kihivyo,
wanatudanganya tu baadhi ya hawa wabunge. Wanasema eti shilingi laki
tatu kwa siku haziwatoshi, kivipi? Nionavyo mimi hata laki moja
kuimaliza kwa siku inahitaji ufujaji wa hali ya juu.
Huwa
haziwatoshi labda wana myanya mingi ya matumizi, labda matanuzi yao ni
ya kujionysha, isije kuwa wanawapa nyinyi madenti. Kataeni.
No comments:
Post a Comment