Yohane Gervas, Rombo MAHAKAMA ya Wilaya ya Rombo imemuhukumu Joseph Didas (39) mkazi wa Kijiji cha Ubaa Tarafa ya Mkuu Wilaya ya Rombo kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili.
Awali mwendesha mashtaka Mkaguzi wa Polisi, Berndad Machibya amedai mahakani hapo kuwa Mshtakiwa mnamo mwezi Julai, 2013 kwa siku nne tofauti alimbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka nane ambaye anasoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Ubaa.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Naomi Mwerinde alisema ameridhika na ushahidi wa pande zote mbili baada ya kusikiliza na kupitia kwa umakini na busara nyingi. Alisema amerithika pasipo na shaka kuwa mshtakiwa Joseph Didasi alifanya kitendo hicho kinyume na kifungu 130, 131 ya kanuni ya makosa ya adhabu.
Aidha Mwerinde alisema uchunguzi wa daktari unaonesha kuwa mlalamikaji alibakwa kwani baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi walibaini kuwepo kwa michubuko sehemu za siri pamoja na rangi nyekundu katika sehemu hizo jambo ambalo si la kawaida.
Kabla ya Hakimu Mwerinde kutoa hukumu hiyo upande wa mashtaka ukiongozwa na mwendesha mashtaka wa polisi Mkaguzi, Bernad Machibya aliomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na wengine wote wenye matendo kama yake, kwani vitendo vya ubakaji kwa watoto wadogo wilayani Rombo vinaonekana kukithiri.
Akitoa hukumu hiyo hakimu Mwerinde alisema kuwa kitendo hicho ni cha kikatili na cha kusikitisha hivyo alistahili kifungo cha maisha lakini kutokana na mshtakiwa kuiomba mahakama na kujitetea kuwa ni mgonjwa imempunguzia adhabu. Hakimu Mwerinde alisema sasa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment