Monday, February 24, 2014
ILE NYONGEZA YA POSHO WANAO DAI WABUNGE WA KATIBA YAGONGA MWABA
Madai ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutaka nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge hilo yamegonga mwamba, Mwananchi limebaini.
Habari kutoka ndani ya kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho ili kufuatilia madai hayo, zimedai kuwa baada ya uchunguzi wa kina, wajumbe wa kamati hiyo hawakuona sababu ya kupendekeza posho hizo kupandishwa.
Taarifa hizo zilidai kuwa wajumbe hao wamefikia uamuzi huo baada ya kupitia viwango vya posho vinavyolipwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali na Mashirika ya Umma.
Pia kamati hiyo ilichambua viwango vya posho walivyolipwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na viwango vya posho ya kujikimu vya Sh80, 000 kwa siku wanavyolipwa watumishi wa Serikali.
“Hili jambo linahitaji busara sana na kutazama mazingira ya nchi pia, kwa hiyo wajumbe wale baada ya kuoanisha viwango vya posho vya taasisi mbalimbali wameona Sh300,000 zinatosha,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Mjumbe mwingine, ambaye pia hakutaka kutajwa, alisema kuwa watakaa leo kukamilisha taarifa ya utafiti wao, kabla ya kuikabidhi kwa Mwenyekiti Kificho.
Alisema pamoja na umuhimu wa kazi za mbunge, lakini isingekuwa rahisi kuongeza posho katika mazingira ya sasa, ambapo wananchi wanalia hali ngumu ya maisha.
Wajumbe hao walioteuliwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho ni William Lukuvi, Mohamed Abood Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari.
Awali, taarifa kutoka ndani ya Bunge zilidokeza kuwa wajumbe hao walikuwa wakutane jana saa 9:00 alasiri ili kuandaa ripoti itakayopelekwa kwa Kificho ikiwa imebeba ushauri kuwa kiwango cha sasa cha posho kinatosha.
Sh300,000 wanazolipwa wajumbe wa Bunge Maalamu la Katiba zinajumuisha Sh80,000 kwa siku ambayo ni posho ya kujikimu na Sh220,000 kwa siku kama posho maalumu ya kuhudhuria kikao.
Posho maalumu ya Sh220,000 inajumuisha posho ya dereva inayopaswa iwe kati ya Sh40,000 na Sh45,000 kwa siku, usafiri wa ndani (mafuta ama teksi), mawasiliano na matumizi mengine binafsi.
Ofisi ya Bunge Maalumu
Alipoulizwa kuhusu jambo hilo mmoja wa makatibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alisema suala la posho linashughulikiwa na Serikali.
“Ninachokifahamu ni kuwa suala la posho limetoka mikononi mwa Kificho na sasa lipo serikalini. Kamati iliyoundwa bado inalishughulikia suala hilo. Hicho ndiyo ninachokifahamu,” alisema Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Kificho, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya kuzungumzia suala hilo, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Hoja ya kutaka nyongeza ya posho iliibuliwa na wajumbe wawili ambao ni wabunge wa CCM waliodai kuwa kiwango cha Sh300,000 wanacholipwa, hakitoshi kwa kile walichodai kuwa ni kuishi Dodoma ni gharama kubwa.
Hata hivyo uchunguzi wa kina umebaini kuwa baadhi ya wajumbe wanaishi katika hoteli za kati ya Sh20,000 na Sh40,000 kwa siku huku baadhi yao wakiishi katika hosteli kwa Sh8,000 kwa siku.
Mmoja wa wajumbe, Augustino Mrema alidai kuwa baadhi ya wajumbe wanataka kuligeuza Bunge hilo ‘shamba la bibi’ kwa kudai posho zaidi kwa kisingizio cha kupanda gharama za maisha.
Mrema alisema kiasi cha Sh300,000 wanacholipwa wajumbe kinatosha kwani zipo hoteli nzuri za kati ya Sh15,000 hadi Sh40,000 ambazo zina hadhi na sifa ya kuishi wajumbe wa Bunge la Katiba.
“Mjumbe ameamua kwenda kuishi chumba cha Sh200,000 wakati akijua atalipwa posho ya Sh300,000 halafu analalamika kupanda kwa gharama za maisha, hizi gharama zimetengenezwa,” alisema Mrema.
Alisema gharama za teksi kutoka bungeni hadi maeneo ya Area C na D haizidi Sh12,000 wakati chakula kinaanzia Sh6,000 hadi Sh20,000 na kuhoji iweje Sh300,000 zionekane hazitoshi.
Hoja ya baadhi ya wajumbe kudai posho zaidi imepigiwa kelele nchi nzima huku wananchi wakimtaka Rais Jakaya Kikwete kulivunja Bunge hilo, kama wataendelea kung’ang’ania kupanda kwa posho.
Mjumbe mwingine wa Bunge hilo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro ameahidi kuanzia leo kukusanya saini za wajumbe wanaopinga suala hili ili ampelekee Rais Kikwete kama ushahidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment