Monday, February 24, 2014

Kidato cha 4 wafaulu zaidi 2013

 
Ramani ya Tanzania
Baraza la Mitihani Tanzania, NECTA limetangaza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2013, ambapo kiwango cha kufaulu kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 15 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2012, ambayo yalisababisha malumbano makali kati ya serikali na wadau wa elimu nchini humo.
Matokeo ya mitihani ya mwaka 2013 yanaonyesha kuwa kiwango cha kufaulu kilikuwa asilimia 58.25, zaidi ya kile cha matokeo ya mitihani ya mwaka 2012 ambapo wanafunzi walifaulu kwa asilimia 43.08
Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania, NECTA, Dr. Charles Msonde amesema kiwango cha kufaulu kwa masomo yote kimeongezeka kwa asilimia 16.72 kutoka asilimia 0.61 ya matokeo ya mitihani ya mwaka 2012.
Dr. Msonde amesema matokeo hayo yanaonyesha kuwa watahiniwa 74,324 ambao ni sawa na asilimia 21.09 wamefaulu kwa madaraja ya kwanza hadi tatu.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa wanafunzi 151,187 ambao ni sawa na asilimia 42.91 wamepata daraja sifuri na 126,828 sawa na asilimia 36 wamepata daraja la nne.
Wanafunzi 404,083 walifanya mtihani huo wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2013.
Wanafunzi wa sekondari katika moja ya shule za Tanzania
Somo la Kiswahili limeongoza kwa wanafunzi kufaulu, likifuatiwa na masomo ya Kemia na Kiingereza.
Hata hivyo matokeo hayo yamelalamikiwa na wadau mbalimbali wa elimu nchini Tanzania, wakisema formula mpya iliyotumika kupanga madaraja imewazesha wanafunzi wengi ambao wangeshindwa mtihani huo kufaulu.
Matokeo hayo yalipangwa kwa kutumia alama zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome mwaka jana. Alama hizo ni A(75-100), B+(60-740, B(50-59), C(40-49), D(30-39), E(20-29) na F(0-19)
Upangaji wa zamani ulikuwa ukitolewa kwa alama A(80-100), B(65-79), C(50-64), D(35-49) na F(0-34)
Upangaji huo wa alama ndio unaolalamikiwa na wadau wa elimu nchini kuwa unalenga kuwahadaa wananchi na wanafunzi wenyewe kuwa matokeo ya mwaka huu ni bora zaidi kuliko yale ya mwaka jana, ilihali kama mfumo wa zamani ungetumika wengi wangefeli.
Shule za binafsi ndizo zimeendelea kuongoza katika kufaulu mitihani nchini Tanzania ambapo shule kumi bora ni za taasisi binafsi na wanafunzi kumi bora ni kutoka pia shule binafsi, saba ni wasichana na watatu ni wavulana.

No comments:

Post a Comment