Tuesday, February 25, 2014

HUYU NDO MGENI RASMI KATIKA MASHINDANO YA KILIMANJARO MARATHON

 
Mhe. Dk. Fenella Mukangara
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dk. Fenella Mukangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mbio mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon ambazo zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya tarehe 2 Machi, 2014 katika uwanja wa MUCCOBS, mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, ambao ndio waratibu wa mbio hizo alisema jana kwamba Dr. Mukangara amekubali kuwa mgeni rasmi na atahudhuria sherehe ya utoaji zawadi ambapo atatoa zawadi kwa washindi kumi wa mbio defu za kilomita 42 maarufu kama Full Marathon kwa wanaume na wanawake. 
Aggrey Marealle
“Uwepo wa waziri ni ishara ya uungaji mkono tukio hili na ameeleza kufurahishwa kwake na maandalizi ya hali ya juu ya Kilimanjaro Marathon. Dk. Mukangara ameeleza mara kadhaa kwamba serikali inaunga mkono Kilimanjaro Marathon kwa kutambua mchango wake michezo, utalii na uchumi,” alisema Marealle.
Marealle aliongeza kwamba baada ya sherehe ya utoaji zawadi Waziri ataungana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na mpenda michezo Mhe. Leonidas Gama, wawakilishi wa wadhamini na watu wengine mashuhuri kwenye mlo maalum  wa mchana uliodhaminiwa na Kibo Palace Hotel. 
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro binafsi na kupitia ofisi yake amekuwa muungaji mkono wa Kilimanjaro Marathon na amekuwa akifurahia kukaribisha maelfu ya watu wanaokuja Moshi kutoka mataifa mbalimbali.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo alisema “mbio za mwaka huu zimesheheni motisha mbalimbali za kuvutia ili kuongeza idadi ya washiriki. Washindi wa kwanza kwenye mbio ndefu za kilomita 42 (Kilimanjaro Premium Lager Marathon) wanawake kwa wanaume watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 4 kila mmoja, shilingi milioni mbili kwa washindi wa pili na shilingi milioni 1 kwa washindi wa tatu. Washindi wa kwanza kwenye mbio ndefu za  nusu marathon (km 21) wanawake kwa wanaume watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 2 kila mmoja, shilingi milioni 1 kwa washindi wa pili na shilingi 500,000 kwa washindi wa tatu.
Waandaaji John Addison wa Wild Frontiers, Mwesiga Kyaruzi wa Executive Solutions na Debbie Harrison
Addison aliongeza kuwa medali na t-shirt zitatolewa kwa wanariadha 500 wa kwanza kumaliza mbio za kilomita 42, wanariadha 2,200 wa kwanza kumaliza mbio za nusu marathon na wanariadha 80 wa kwanza kumaliza mbio za walemavu.  Washiriki 3,000 wa kwanza kumaliza mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run watapewa t-shirts baada ya kumaliza mbio na watapata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali za kuvutia kupitia droo.

Mbio hizi zinaratibiwa na kwa kushirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, Kibo Palace Hotel, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.

No comments:

Post a Comment