Monday, May 20, 2013

NGASSA AKATAA MAMILIONI YA SIMBA


Na Mwandishi Wetu
JUHUDI za Simba kutaka kuona kiungo Mrisho Khalfan Ngassa anaifunga Yanga juzi zilikwama pamoja na kumuahidi mamilioni ya fedha kama angefunga bao katika mechi hiyo ya watani.

Katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Simba kulala kwa mabao 2-0, Ngassa aliahidiwa kulipwa Sh milioni tatu kwa kila bao atakalofunga, lakini yeye hakufanya hivyo, badala yake akasisitiza yeye ni “Yanga damu.”
“Simba walimuahidi Ngassa shilingi milioni tatu kwa kila bao ambalo angefunga dhidi ya Yanga, alikubaliana nao lakini akaniambia asingeweza kufanya hivyo kwa kuwa yeye ni Yanga damu,” alieleza ndugu yake na Ngassa ambaye hakutaka kutajwa.

Baada ya kukataa mamilioni hayo ya Simba na kuepuka kuifunga Yanga, Ngassa amemuambia mwandishi wetu, Wilbert Molandi kwamba sasa yeye ni mchezaji halali wa Yanga.

“Kweli mimi ni mchezaji wa Yanga na nimesaini mkataba wa miaka miwili, nisingeweza kusema hivyo wakati nilikuwa bado niko Simba. Nilikuwa nina hofu ya kubanwa na kanuni, lakini sasa nipo huru,” alisema Ngassa.
Championi lilikuwa la kwanza Jumatano kuandika kuhusiana na Ngassa kusaini Yanga mkataba wa miaka miwili, hali iliyofanya Simba wacharuke wakionyesha kutokuwa wazi, lakini walikuwa hawakubaliani na hali hiyo.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Yanga, mchezaji huyo atatambulishwa leo kwenye moja ya hoteli za kisasa.
“Utambulisho huo utafanyika mbele ya waandishi wa habari na kwa mara ya kwanza atazungumza mbele yao na kuelezea kutua kwake Yanga,” kilieleza chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga.

Kumekuwa na taarifa kwamba Ngassa amesaini mkataba na Simba, ndiyo maana alipewa gari na Sh milioni 30, lakini mchezaji huyo amekuwa akikanusha kuhusiana na hilo.
Ngassa ambaye alijiunga na Azam FC kwa mkopo akitokea Yanga, amerejea Yanga ambayo ilimuuza Azam FC kwa Sh milioni 98, miaka minne iliyopita.

Yanga ilimsajili kutoka Kagera Sugar ambayo alijiunga nayo akitokea Toto African ya Mwanza, mji ambao alizaliwa na kujifunza soka kama ilivyokuwa kwa baba yake mzazi, Khalfan Mrisho Ngassa aliyewahi kucheza Pamba, Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.

No comments:

Post a Comment