Friday, May 10, 2013

Hizi ndizo alama za Benitez Chelsea

 

 

 
In Summary
WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa kuwa kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho atatua Chelsea, Julai Mosi, hiyo inamaanisha Rafa Benitez atalazimika kupishana naye mlangoni.
WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa kuwa kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho atatua Chelsea, Julai Mosi, hiyo inamaanisha Rafa Benitez atalazimika kupishana naye mlangoni.
Hata hivyo miezi sita ya Benitez pale Chelsea imekuwa na maana kwenye klabu na huenda jambo hilo likamfanya kocha mpya apate mteremko.
Kwanza alitua kwenye klabu hiyo huku kila shabiki akikunja sura kuashiria kuwa hawakupenda kumuona kocha huyo hasa kwa kuwa kuna historia mbaya kati ya Chelsea na Liverpool aliyokuwa akiifundisha zamani.
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, alifumba macho na kumpa kazi kocha huyo licha ya kwamba mashabiki walikuwa bado wanamkubali Roberto Di Matteo.
Sasa kocha huyo anakaribia kuondoka kwenye klabu yake huku akiwa ameacha mtazamo tofauti, timu ambayo ilikuwa haina uhakika wa kutua kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya sasa inakaribia kutua hapo, timu imetua kwenye fainali ya Ligi ya Europa na kikosi chake si cha mchezo kwani kinaweza kuitibulia safari timu yoyote kubwa. Kocha huyo ametoa mapinduzi kwa kufanya haya;
 David Luiz kuwa kiungo
Kabla ya msimu huu David Luiz alikuwa akicheza nafasi ya beki, lakini Benitez aliamua kumpa nafasi ya kiungo.
Mchezaji huyo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimudu nafasi hiyo na hivyokuifanya timu ichangamke zaidi na kupata mafanikio haraka.
Jambo hilo limetoa mwanya kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kujaribu kufunga kwa umbali mrefu, mfano mzuri ni wakati alipofunga bao kwenye mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Europa dhidi ya Basel na pia aliwahi kufunga bao la mita 30 kwenye mechi dhidi ya Fulham msimu huu.
Awali mchezaji huyo alionekana hana kiwango kikubwa akiwa nyuma, lakini kwa wakati huu amekuwa tishio.
Torres ameanza kukubalika
Ingawa Fernando Torres hajafikia kiwango chake cha siku za nyuma, angalau Benitez amemsadia na kuanza kurudisha chenji kufuatia kusajiliwa kwa ada ya pauni 50 milioni kutoka Liverpool na kushindwa kutamba.
Torres na Benitez wote ni raia wa Hispania labda hiyo ndiyo ilifanya kocha huyo afahamu mchezaji huyo anatakiwa kucheza vipi.
Msimu huu mchezaji huyo amefunga mabao 21 kwenye mechi 60, tofauti na msimu uliopita ambapo alifunga mabao 11 pekee. Torres hajafanya vizuri sana, lakini angalau amerudisha ari uwanjani.
Kaonyesha uthubutu
Ukweli ni kwamba wakati Roberto Di Matteo alipotimuliwa kwenye kikosi Novemba mwaka jana, makocha wenye majina makubwa hawakutamani kujiunga na klabu hiyo.
Mmiliki wa klabu alijaribu kutafuta makocha wazuri lakini walikataa. Licha ya kumuahidi donge nono kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola kocha huyo alikataa kujiunga na klabu hiyo ya bilionea huyo wa Russia.
Wengi walikuwa wakiogopa kufika na kutimuliwa na kibaya ni kuwa timu ilikuwa na wakongwe wengi na haikuwa na ubunifu mpya.
Lakini Benitez ameweka mambo sawa, na tayari makocha wakubwa kama Jose Mourinho, Manuel Pellegrini na David Moyes wanatamani kufika hapo. Sababu nyingine iliyofanya makocha waogope kutua ni ukweli kwamba ulikuwa mwaka mgumu kwa Chelsea.
Timu ilikuwa kwenye mashindano ya Kombe FA, Kombe la Ligi, Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi ya Europa na Klabu Bingwa ya Dunia. Makocha walikuwa wakiogopa kutimuliwa baada ya kukosa vikombe vyote.
  Uvumilivu
Kocha huyo alionyesha nguvu kubwa baada ya kudharau matusi ya mashabiki uwanjani. Wakati alipochukua timu mashabiki walimchukia sana na kelele zao ziliwafanya hata wachezaji wakose ari uwanjani.
Hata hivyo kocha huyo hakukata tamaa, aliendelea kuijenga timu na hakujibu mashambulizi ya mashabiki hata siku moja.
Kocha huyo pia alikuwa na matatizo nje ya uwanja. Amekuta wachezaji wakubwa ambao walikuwa bora chini ya Mourinho. Wakongwe kama John Terry na Frank Lampard walitamba siku za nyuma lakini kwa wakati huu viwango vinaanza kupotea. Benitez alianza kwa kuwapunguzia mechi na kutoa nafasi kwa damu changa.
Jambo hilo lilizua mzozo kwenye klabu lakini Benitez alifumba macho na kuendelea na kazi yake. Kuna wakati Benitez alijaribu kuwaambia Lampard na Terry kwamba wakati wao umepita na aliona wazi kuwa uamuzi wa kuwapanga Oscar, Juan Mata na Eden Hazard ulikuwa sahihi kwake.

No comments:

Post a Comment