NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analipwa sh milioni 384 kwa mwaka, sawa
na sh milioni 32 kwa mwezi pasipo kukatwa kodi.
Hii ni mara ya pili kwa Zitto
kutangaza hadharani mishahara ya viongozi wakuu wa serikali, akiwa
ameanza na ule wa Waziri Mkuu, aliyesema analipwa takribani sh milioni
26 kwa mwezi.
Akiwahutubia wananchi mjini Igunga
jana, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama Kanda ya
Magharibi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema kuwa
sababu ya kutaka mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ijulikane, ni
kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo
hilo.
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi
wanacholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi, bali ni usiri
unaofanywa juu ya kiwango hicho jambo alilosema kuwa linaweza kutumiwa
na wajanja kuendelea kuinyonya nchi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona
mwalimu anayelipwa mshahara wa sh 220,000 kwa mwezi akikatwa kodi, huku
viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo
kukatwa kodi licha ya kuhudumiwa kila kitu na serikali.
Aliongeza kuwa katiba ya sasa Ibara
ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara pamoja na malipo mengine,
huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupurupu
kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha
sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk.
Willibrod Slaa akiwa rais na akataka kupunguza mshahara wake, kwa katiba
hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi
wanapata kila kitu bure kutoka serikalini,” alisema Zitto.
Akiwa katika Kata ya Choma, Zitto
alikagua kilichokuwa kiwanda cha kuchambulia pamba cha Giner ambacho
kimeacha kufanya kazi tangu mwaka 1998.
Alisema kufa kwa viwanda vingi vya
uzalishaji nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Rais
mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, akidai kuwa alishindwa
kutofautisha suala la uwekezaji na biashara huru.
“Ni serikali ya Mkapa ndiyo
ilitufikisha hapa katika kupotea kwa viwanda nchini, wao walidhani
biashara huru ni kuwapa wawekezaji viwanda vyetu na serikali kujiweka
pembeni, sasa nchi imebaki kutegemea uchumi wa uchuuzi badala ya
uzalishaji,” alisema.
Alisema sera ya uwekezaji katika
Serikali ya CCM ilichukuliwa kama fursa ya viongozi wa chama hicho
kujinufaisha na mali za serikali pasipo kujua wataendeleza vipi.
Zitto alisisitiza kuwa kila mara
CHADEMA imekuwa ikisisitiza bungeni juu ya kupiga marufuku usafirishaji
wa pamba kwenda nje kama malighafi, na badala yake wakitaka viwanda
vifufuliwe kwa ajili ya kutoa ajira kwa Watanzania.
Alirejea kusisitiza sera ya hifadhi
ya jamii kwa wakulima akisema imefikia wakati serikali kupitia SSRA ione
umuhimu na ulazima wa kuhakikisha wanaongeza Watanzania wenye hifadhi
ya jamii kwa kuanza mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa wakulima
(Supplementary scheme for social security to small holder farmers).
“Ninapendekeza serikali ichangie nusu
kwa nusu na mkulima ili kuvutia uwekaji akiba katika nchi na kuwa na
sera ya uwekezaji katika maeneo yatakayomwinua mkulima kama miundombinu
ya umwagiliaji, mikopo nafuu kwa wakulima kwenye pembejeo na nyumba na
bima ya afya.
“Nimezungumzia umuhimu wa uwazi
katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi
wa umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega kuwa siku ya Jumanne kamati
yangu ya Hesebu za Serikali (PAC) itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya
siasa nchini,” alisema.
Zitto alisema vyama vya siasa
vinatumia fedha za umma takribani sh bilioni 20 kila mwaka kama ruzuku,
kwamba ni haki ya wananchi kujua fedha zinatumika namna gani.
Alisema kuwa wananchi wa Nzega wana
changamoto nyingi sana. Kwamba wakulima wa pamba walipewa madawa feki ya
kuua wadudu, michango ya hovyo hovyo ni mingi mno na unyanyasi wa
wana-CHADEMA ni mkubwa vijijini.
-Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment