Saturday, October 26, 2013
CCM WASUTANA DODOMA-WANYOOSHEANA VIDEOLE MATUMIZI YA PESA
*Mada ya rushwa yaibua malumbano Dodoma
*Wagombea wanyoosheana vidole matumizi ya fedha
BAADHI ya wanasiasa wanaotajwa kutaka kuwania ukuu wa dola mwaka 2015 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ), sasa wanadaiwa kusababisha malumbano makali kando ya semina ya mafunzo ya utendaji, yanayowahusisha Wenyeviti na Makatibu wa wilaya na mikoa wa chama hicho, iliyomalizika jana mjini Dodoma.
RAI limedokezwa kuwa malumbano hayo yametokana na kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuitumia semina hiyo kama njia ya ushawishi kwa kutoa rushwa ili kujijengea mazingira ya kuteuliwa kuwa wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2015, hali iliyowaibua baadhi ya makada wa chama hicho ambao wamewanyooshea vidole vigogo hao.
Habari zilizolifikia RAI kutoka ndani ya semina hiyo iliyohitimishwa jana na Rais Jakaya Kikwete mjini Dodoma, zimeeleza kuwa baadhi ya wajumbe, waliwashambulia kwa maneno makali makada wenzao kuwa tamaa yao ya uongozi inayowasukuma kutumia fedha nyingi kutafuta uungwaji mkono, inakichafua chama.
Mmoja wa wajumbe wa semina hiyo aliyezungumza na gazeti hili (jina lake tunaliifadhi) alisema kuwa, yaliibuka malumbano makali wakati mmoja wa mawaziri vijana na kada wa CCM mwenye ushawishi kwa vijana alipokuwa akiwasilisha mada yake iliyohusu mwelekeo wa CCM na taswira ya wapiga kura katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Inaelezwa kuwa katika mada hiyo, Naibu Waziri huyo kijana alieleza namna CCM kilivyoanza kupoteza mwelekeo na mvuto kwa wapiga kura kwa sababu ya uwepo wa makundi ya wanachama wake wanaotumia fedha kusaka uongozi.
Mtoa habari huyo alieleza kuwa kauli ya waziri huyo ambaye pia amekuwa akitajwa kuendesha mikakati ya chini kwa chini ya kutafuta uungwaji mkono kwa ajili ya kuwania urais 2015, iliibua malumbano kando ya ukumbi wa semina na baadhi ya wajumbe wakimnyooshea kidole kuwa hata yeye anatuhumiwa kutumia fedha katika harakati zake.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu, baadhi ya wajumbe walihoji alikopata uhalali wa kuzungumzia jambo hilo ili hali yeye mwenyewe ameutumia mkutano huo kugawa rushwa ya Sh 50,000 kwa makatibu 50 na wenyeviti 50 wa baadhi ya mikoa na wilaya.
Haikufahamika mara moja waziri huyo kijana alikotoa fedha hizo, lakini taarifa zaidi kutoka ndani ya semina hiyo zinaeleza kuwa kuna idadi kubwa ya wapambe wa watu waliokwishaonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, ambao wamekuwa wakijipitisha kwa wajumbe wa mkutano huo na kuwagawia fedha.
RAI limetajiwa majina ya vigogo wawili wa CCM wenye asili ya Kanda ya Ziwa ambao wapambe wao wameonekana wakiwapatia bahasha za kaki baadhi ya wajumbe ambao baada ya kuzifungua wamekaririwa wakieleza kukuta fedha ndani.
Mmoja wa vigogo hao anatajwa kuwa ni waziri mwandamizi katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, naye anamtumia mmoja wa wabunge wa mkoa wake kugawa kiasi cha Sh 200,000 kwa wajumbe aliokwishawafikia.
Inaelezwa kuwa mpambe huyo wa Waziri aliibua malalamiko kutoka kwa wajumbe wa Zanzibar, ambao hakuwapatia fedha na walipomhoji ni kwanini anawabagua katika mgawo huo, alijibu kuwa hakupewa majina yao lakini watu walio karibu naye wameeleza kuwa Wazanzibari hawapo kwenye mgao kwa sababu hawana nguvu ya ushawishi katika vikao vya uteuzi vya wagombea urais.
Mbali na waziri huyo, anatajwa pia aliyepata kuwa waziri katika moja ya wizara nyeti kabla ya kufanyika kwa mabadiliko ya baraza la mawaziri, ambayo yalimuacha pembeni kuwa naye ametuma wapambe wake katika semina hiyo ambao wamekuwa wakiwafikia wajumbe wa semina hiyo kwa kuwaomba wamuunge mkono katika nia yake ya kuwania urais mwaka 2015.
Wapambe hao wa mwanasiasa huyo kijana, ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na pia walikuwa wabunge katika Bunge lililopita ambao wanawagawia wajumbe wanaowafikia bahasha zenye Sh 100,000 hadi Sh 150,000 ili kuhakikisha mgombea wao anaungwa mkono wakati utakapofika.
Jitihada za gazeti hili kumpata Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahiman Kinana kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita muda mrefu bila kupokelewa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment