Mshtakiwa Makongoro Nyerere
anayekabiliwa na kesi ya mauaji pamoja na Mfanyabiashara maarufu
Abubakar Marijan [50] maarufu kama Papaa Msofe, amedai mahakamani kuwa
amebambikiwa kesi hiyo.
Kadhalika alidai kuwa mahakama ikipitia jalada la kesi hiyo itabaini kwamba amebambikiwa kesi hiyo.
Nyerere alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Hellen Riwa.
“Mheshimiwa hakimu, mahakama
ikilipitia jalada la kesi hiyo kwa umakini, utabaini kwamba mimi
sikuhusika na mauaji, nimebambikiwa baada ya askari polisi kuniomba
rushwa ya Sh. milioni 8... nilipowakatilia kuwapa wakaamua kunipa kesi
hii,” alisema Nyerere.
Alidai kuwa pamoja na mawakili wa
upande wa Jamhuri kuwa ni wasomi wazuri, lakini wanafanya mambo yao
tofauti na elimu waliyonayo na wanasabisha ateseke mahabusu bila sababu.
Hakimu Riwa alisema kwa kuwa upande
wa Jamhuri umedai upelelezi bado haujakamilika, kesi hiyo itatajwa
Oktoba 31, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa
washtakiwa wote kwa pamoja walimuua kwa makusudi Onesphory Kituli,
kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu sura ya 19 kama
kilivyofanyiwa marekebisho mwaka, 2002.
Ilidaiwa kuwa, Oktoba 11, 2011, nyumbani kwake Kituli, Magomeni Mapipa, wilayani Kinondoni washtakiwa walitenda kosa hilo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mwenendo wa
Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), washtakiwa hawakutakiwa kujibu
chochote hadi upalelezi utakapokamilika kesi yao itahamishiwa Mahakama
Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment