Friday, October 25, 2013
INASIKITISHA SANA! MTOTO AMBAYE NDUGU ZAKE WALITAKA AUAWE, AFARIKI DUNIA
INAUMA SANA! Yule mtoto ambaye Amani liliripoti kuwa ndugu wanataka auawe wiki iliyopita, Mwajuma Haji (16), amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar.
Mwanyuma alikuwa na ugonjwa wa kusinyaa na vipimo vya madaktari havikuonesha ugonjwa uliokuwa ukimsumbua, ingawa viungo vyake vyote vilikuwa vimesinyaa na kujikunja tangu alipozaliwa. Kutokana na tatizo hilo, baadhi ya ndugu walifikia hatua ya kutaka auawe kwa walichodai alikuwa mzigo kwa familia.
Akizungumza na mwandishi wetu kwenye mazishi ya mtoto huyo kijijini kwao Kimange, Wilaya ya Bagamoyo, Tatu alisema mwanaye alizidiwa kwa siku tatu mfululizo huku akiwa anapumulia mashine kabla mauti hayajamkuta. Alisema madaktari walijitahidi kwa hali na mali kuokoa maisha yake lakini ilishindikana kwani alikuwa akipumua kwa shida. “Mwanangu ameteseka sana dakika za mwisho kwani kwa siku tatu mfulululizo alikuwa akipumulia gesi tu mpaka Mungu alipomchukua,” alisema mama huyo. Katika mazishi ya mtoto huyo, waliokuwa karibu na mama Mwajuma ni majirani zake baada ya ndugu kuingia mitini.
Majirani wa karibu na mama Mwajuma waliliambia Amani kuwa wanasikitishwa na tabia za ndugu zake waliosusia msiba huo na kudai ndiyo tabia yao kwani kipindi Mwajuma alipokuwa hai walikuwa hawamjali hata walipomkuta akinyeshewa mvua hawakumuingiza ndani hadi mama yake alipofika. “Tabia za ndugu wa mama Mwajuma hazijaanza leo kwani walikuwa wakimtenga sana mtoto huyo kwa kuwa hata walipomkuta ananyeshewa na mvua walikuwa wakimuacha hadi mama yake arudi,” alisema jirani mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment