Tuesday, October 29, 2013
UWEZI AMINI TANZANIA IMETEGWA TENA KATIKA MKUTANO WA EAC
NCHI za Tanzania na Burundi, kwa mara nyingine zimetengwa na wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya marais wa Kenya, Uganda na Rwanda kukutana mjini Kigali jana. Marais hao walitarajia kujadili namna ya kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia uimarishwaji wa miundombinu, uchumi, biashara pamoja na kuweka mikakati ya shirikisho la kisiasa.
Kitendo cha kuziacha Tanzania na Burundi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kinazidi kutia shaka mtangamano wa jumuiya hiyo.
Nchi hizo mbili zimeshaeleza kusikitishwa na muungano wa nchi hizo tatu, ambao zimesema unakwenda kinyume cha makubaliano na mkataba wa EAC.
Katika mkutano huo, marais hao, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya, pamoja na mambo mengine, walitarajia kusaini makubaliano ya kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya ushuru kinachotarajia kurahisisha uchukuzi wa bidhaa kutoka Mombasa nchini Kenya, Uganda hadi Rwanda.
Aidha Sudan Kusini ilialikwa ikiidhinishwa kama mshirika katika kikao hicho.
Mkutano huo unakuja baada ya ule uliofanyika mjini Kampala, Uganda, Juni mwaka huu na mwingine uliofanyika Mombasa, Agosti, ambako viongozi hao watatu walipendekeza kupanuliwa kwa Bandari ya Mombasa, ili kuwezesha uharaka wa bidhaa kupitishwa katika kuhudumia kanda nzima.
Mkutano mwingine wa marais wa nchi 15 za Afrika, ikiwamo Tanzania, utafanyika leo nchini hapa, katika kongamano la siku nne ambalo linatarajiwa kuweka kipaumbele kwa uimarishwaji wa huduma za internet katika mataifa hayo.
Kwa mujibu ya waandaaji, zaidi ya wajumbe 1,500 watahudhuria mkutano huo, chini ya uenyeji wa Rais Paul Kagame na Dk. Hamadoun I. Toure, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano ya Kiteknolojia (ITU).
-Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment