Friday, October 11, 2013

NGASSA ARUDI AZAM, AUNGANA NA MWAIKIMBA



Na Khatimu Naheka
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa ameikumbuka timu yake ya zamani ya Azam FC baada ya kuonekana akiwa kwenye Uwanja wa Chamazi Complex nje ya jiji la Dar es Salaam.
Ngassa, ambaye awali aliuzwa na Yanga kwenda Azam FC kwa kitita cha pauni milioni 98, miaka mitatu iliyopita kabla ya kurudi msimu huu, juzi alitua kwenye Uwanja wa Chamazi na kushuhudia mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji na Mgambo Shooting.
Ngassa aliyeondoka Azam FC kwa mgogoro huku timu hiyo ikimpeleka Simba, alikuwa kivutio na wengi walianza kuonyeshana alipokuwa amekaa jukwaani.
Baada ya kufika uwanjani hapo, moja kwa moja Ngassa alikwenda kukaa alipokuwa amekaa mshambuliaji wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba waliyewahi kukipiga pamoja Jangwani.
Mara baada ya mechi hiyo, kiungo huyo aliyerudi kwa kasi katika Klabu ya Yanga, kwa kuifungia bao moja mpaka sasa, alisalimiana na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo na kuondoka zake.
Ngassa alipoulizwa sababu za kwenda uwanjani hapo alisema kwa ufupi: “Nimekuja kutembea tu.”

Tayari Ngassa yupo mjini Bukoba kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji Kagera Sugar, kesho.

No comments:

Post a Comment