Wednesday, August 21, 2013

Godbless Lema augua ghafla, kesi yake yaahirishwa


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha jana imeshindwa kuanza kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kutokana na mbunge huyo kuwa mgonjwa.
Wakili wa Lema, Method Kimomogoro, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Hawa Mguruta, anayesikiliza shauri hilo kuwa Lema anaumwa na alikuwa amelazwa katika Hospitali ya AICC tangu Agosti 14 hadi 19, mwaka huu aliporuhusiwa kutoka hospitali, hivyo ametakiwa apumzike kwa muda wa siku 10 kuanzia Agosti 19, mwaka huu.
 
Wakili Kimomogoro aliomba shauri hilo liahirishwe hadi siku nyingine, ombi lililokubaliwa na hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 1 na 2 mwaka huu, ambapo mashahidi tisa wanatarajiwa kutoa ushahidi wao.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Swai, anayesaidiana na Mary Lucas, alikubaliana na ombi hilo na kuongeza kuwa mashahidi wanne miongoni mwa tisa walikuwapo mahakamani hapo kutoa ushahidi wao jana ambao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha (OCD) Gilles Mroto, Naibu Mkuu wa Chuo cha IAA, Faraji Kasidi, Mhadhiri wa chuo hicho, John Nanyaro na maofisa wa Polisi, Jane Chiguga na Bernard Nyambalya.
 
Mashahidi wengine wanaotarajiwa kuletwa mahakamani hapo na upande wa serikali ni pamoja na maofisa wa Jeshi la Polisi,  PC Godfrey, Joachim Mahanyu  na wengine  kutoka Chuo cha Uhasibu, ambao ni  Benjamin Simkanga na Naibu Hamidu.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa  mnamo Aprili 24, mwaka huu, mshitakiwa Lema akiwa eneo la Freedom Square ndani ya Chuo cha Uhasibu, alitoa maneno ya uchochezi yaliyosababisha uvunjifu wa amani.
 
Maneno hayo ni  kinyume cha kifungu cha 390 sura ya 35 cha sheria ya kanuni ya adhabu marejeo ya mwaka 2002 .
“RC anakuja (Chuo cha Uhasibu) kama anaenda kwenye sendoff, hajui chuo kilipo, wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hicho ….. (RC), ameshindwa hata kuwapa (wanafunzi) pole kwa kufiwa na amesema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu,” yalinukuliwa baadhi ya maneno aliyodai kuwa yalitamkwa na Lema siku hiyo.
Kauli hizo zinadaiwa zilipandisha hasira za wanafunzi ambao walianza kumrushia mawe na chupa Mkuu wa Mkoa, Mulongo, alipokuwa akiwahutubia kuhusiana na tukio la kifo cha mwanafunzi, Henry Koga, kilichotokea Aprili 23, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment