SIKU mbili baada ya serikali kutumia
sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inayolalamikiwa na wadau wa sekta ya
habari kuyafungia magazeti mawili ya kila siku ya Mwananchi na
Mtanzania, wadau mbalimbali wamejitokeza na kuipinga adhabu hiyo.
Sheria hiyo inampa ruhusa waziri mwenye
dhamana ya habari kupiga marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote
ambalo anafikiri liko kinyume na maslahi ya umma.
Katika adhabu hiyo, gazeti la Mtanzania
limefungiwa kwa siku 90 huku Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, adhabu
mbazo zimeanza Septemba 27, mwaka huu, yakidaiwa kuchochea.
Wakizungumzia adhabu hizo, wadau hao,
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), mhadhiri mstaafu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama, Mbunge wa Ubungo,
John Mnyika (CHADEMA) na mwandishi nguli, Ndimara Tegambwage walidai
kuwa serikali imeendelea kutumia sheria mbovu kubana uhuru wa habari
nchini.
Zitto: JK amezidiwa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Zitto alisema kuwa serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia
sheria ya kidikteta ya magazeti ya mwaka 1976, ambayo Tume ya Jaji
Francis Nyalali iliiorodhesha kama sheria kandamizi.
Alisema kuwa sababu zilizotolewa
kuhalalisha uamuzi huu hazina maana, na kwamba serikali ingeweza
kufungua mashitaka ya kawaida mahakamani kushitaki magazeti hayo iwapo
haikupendezwa na habari walizochapisha.
“Moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti
la Mwananchi ni kuchapisha taarifa kuhusu mishahara ya serikali.
Serikali inasema habari hii ni siri.
“Serikali hii hii ambayo imesaini
makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi (Open Government Initiative)
na kumwagiwa sifa na Rais Barack Obama wa Marekani, inalifungia gazeti
kwa kuandika habari za mishahara ya watumishi wa serikali,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa mishahara kuanzia wa rais hadi mtendaji wa kijiji haipaswi kuwa jambo la siri.
“Kwamba kuonyesha kuwa jambo hili
linapaswa kuwa wazi, mkutano ujao wa Bunge tutatafuta kila namna kutaja
mshahara wa rais, makamu wa rais, waziri mkuu na baadhi ya watendaji wa
mashirika makubwa ya umma kama njia ya kuwaunga mkono gazeti la
Mwananchi kwa habari yao hiyo,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, mapato ya mbunge
yanajulikana sasa kuwa ni sh milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya kuongeza
posho za vikao za sh 200,000 kwa siku na posho ya kujikimu ya sh 130,000
kwa siku.
“Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao. Tutaanza na mshahara wa rais,” alisema.
Alisema kuwa gazeti la Mtanzania
limefungiwa pamoja na mambo mengine kwa kuandika ‘mapinduzi ni lazima’.
Kwamba inashangaza Serikali ya CCM inaogopa neno mapinduzi.
“Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde,
aliyekuwa mbunge wa Tandahimba alipata kusema bungeni kuwa ‘lazima nchi
ipinduliwe’. Ni matumizi ya lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa
analalamikia maendeleo duni ya mikoa ya kusini na kutaka kaskazini iwe
kusini na kusini iwe kaskazini,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa serikali inafungia
gazeti kwa sababu ya kuandika ‘Mapinduzi ni lazima’ ilhali kila siku
Zanzibar wanasema ‘Mapinduzi daima’.
“Gazeti la Mtanzania linahaririwa na
Absalom Kibanda, mwandishi wa habari ambaye bado anaponya majeraha ya
mwili na kisaikolojia ya kuteswa na watu ambao hadi leo hawajakamatwa.
“Badala ya serikali kuwakamata watesaji
wa Kibanda, inamnyima kazi Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa kukaa miezi
mitatu bila kazi,” alisema.
Pia aliongeza kuwa inawatesa Watanzania
kwa njaa ya kupata habari ambayo ni haki ya msingi ya kikatiba. Kwamba
hiyo ndiyo zawadi serikali inampa Kibanda baada ya kung’olewa kucha,
kunyofolewa jicho, kukatwa vidole na kuteswa kwa namna isiyoelezeka.
“Matukio ya hivi karibuni na namna
serikali inavyoyachukulia yanaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete
kazidiwa nguvu na kundi la wahafidhina ndani ya chama na serikali yake.
“Rais ambaye alianza kwa kuhubiri
uvumilivu wa hali ya juu, na hata yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu
huu wengine wanauona kama udhaifu, lakini ameamua kujenga taifa la
kutovumiliana,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, rais alipata
kulalamika hadharani kwamba kuna wenzake wanataka aongeze ukali, hivyo
ni dhahiri kundi hili la wahafidhina sasa ndilo linalomwongoza Rais
Kikwete.
“Kitu kimoja tu rais azingatie, kundi
hili linaongozwa na maslahi binafsi ya kubakia kwenye utawala wakati
yeye anapaswa kuacha ‘legacy’,” alisema.
Alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atakuwa rais karatasi (lame duck) tu tunapoelekea mwisho wa utawala wake.
Kwamba uamuzi wa hovyo na wa kidikteta wa kufungia magazeti unamchora vibaya mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa.
“Wananchi sasa waifanye serikali kujutia
uamuzi wake wa kufungia magazeti. Nimeamua mimi binafsi kama mbunge
(leo Septemba 30, 2013) kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya
kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa sheria kandamizi ya magazeti
ya mwaka 1976,” alisema.
Ndimara anena
Katika andiko lake kwenye mtandao wa
kijamii, mwandishi wa habari nguli, Ndimara Tegambwage alisema kufungia
magazeti ni uhalifu dhidi ya haki.
Alisema: Serikali inaendelea kufungia vyombo vya habari. Orodha inaongezeka. Mara hii ni zamu ya Mwananchi na Mtanzania.
MwanaHALISI lilifungiwa miezi 15
iliyopita (mwaka mmoja na robo). Hakuna dalili za kulifungulia. ‘Redio
mbao’ zinasema hata wamiliki wake wasiruhusiwe kuanzisha gazeti jingine.
Limekuwa suala la binafsi.
Hatua ya serikali ya kufungia gazeti
hilo imeathiri na inaendelea kuathiri waandishi, wake/waume zao na
watoto wao; wazazi wao, ndugu waliowategemea, wauza magazeti, wenye
maduka karibu na ofisi za gazeti hili, wauza matunda, mihogo, karanga,
kahawa na kashata waliokuwa wakitua MwanaHALISI.
Wengi wameathirika hivyo kiuchumi. Sasa
waandishi wamekuwa wabangaizaji kwa kuomba vibarua katika magazeti ya
wengine. Wananchi wengi wameathirika kwa njia ya kukosa taarifa.
Mtu mmoja serikalini au kundi la watu;
wanatumia nafasi zao kutaka kuua kwa njaa waandishi na familia zao; na
kunyima wananchi taarifa muhimu zinazowawezesha kupata uelewa juu ya
wanavyotawaliwa na jinsi ya kujinasua kutoka mkenge wa ghiliba, wizi na
ufisadi.
Jana serikali iliongeza machungu kwa
waandishi na wananchi na orodha yote niliyotaja hapo juu kwa amri ya
kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania. Na serikali inajua. Hiyo
siyo njia sahihi ya kutenda kazi. Serikali inaingilia kazi na majukumu
ya mahakama.
Kwa ufupi, serikali inapuuza na kudharau
mahakama. Kuna sheria ya magazeti ya mwaka 1976, katili kama ilivyo,
lakini bado inatumika na watawala ndio wameiweka mbelekoni. Kwanini
serikali haiitumii kwa njia ya kwenda mahakamani? Inaogopa nini? Woga
wake ni upi?
Kuna Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Limejaa na linashirikisha wataalamu wa nyanja muhimu katika tasnia hii -
waandishi wa habari na wanasheria. Lina uwezo mkubwa wa kusikiliza na
kutolea uamuzi malalamiko ya mtu au taasisi yoyote. Serikali
hailitumiii.
Wahusika ndani ya serikali wanatumia
ubabe wa amri kwa nia ya ‘kuua sisimizi kwa kutumia nyundo’, lakini nje
ya mkondo wa sheria au ushauri wa kitaaluma ambao unaheshimika zaidi
kuliko amri au mitulinga.
Kesho serikali itazima gazeti au chombo
kingine cha habari. Itaondosha ajira za waandishi. Itafinyaza fursa za
kujiendeleza katika taaluma hii. Itanyakua haki ya uhuru wa kupata
taarifa na habari.
Itafanya kazi zake gizani na kwa hiyo
bila mrejesho kutoka kwa jamii pana iliyokuwa inapata taarifa kupitia
vyombo vya habari vinavyofungiwa.
Kufungia au hata kufuta chombo cha
habari, licha ya kwamba ni kuvunja haki za binadamu; vilevile ni kuziba
mifereji ya fikra ya jamii; kuongeza umasikini, kuasisi woga miongoni
mwa watu, kujenga visima vya chuki na hasira dhidi ya serikali; kutaka
watu waishi kwa umbeya na kurudisha jamii katika ujima.
Hatupendi kuamini kuwa haya yanatendwa
na serikali inayojiita ya ‘kidemokrasia’ na inayojigamba kuwa na uwazi
na utawala bora. Hapana! Kuna serikali ngapi - moja itende demokrasia na
nyingine itende uhalifu dhidi ya haki ya uhuru wa habari? Ghiliba!
Tumependekeza tangu 1985. Kwamba
serikali iache wananchi na waandishi wa habari waiseme wanavyoiona. Kama
sivyo ilivyo, basi ipuuze. Kama ndivyo ilivyo, basi ijisahihishe.
Serikali ina maguvu mengi ya kutumia
kuleta mabadiliko kwa maslahi ya watu; na siyo kwa kuangamiza uhuru wa
kufikiri na kutoa mawazo. Inakokwenda serikali, siko!
Lwaitama
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Dk. Lwaitama alisema si sahihi kufungia magazeti na serikali
kuanza kupangia wananchi wasome au wasisome nini.
“Tunaomba tuambiwe mahojiano hayo na
maonyo yalifanyika chini ya uangalizi wa nani? Na yalifanyikia wapi?
Hapa ninaona kuna kikundi kidogo cha watu fulani katika serikali
wameamua kuanza kufungia magazeti kwa manufaa yao,” alisema.
Dk. Lwaitama aliongeza kuwa tuhuma
zinapotolewa zipelekwe kwenye chombo cha uamuzi ili hukumu itolewe,
kwamba haiwezekani serikali ndiyo inatoa tuhumu na kuhukumu yenyewe.
“Tumekuonya, hatupendezwi na uandishi
wako, hivyo tunakufungia siku 14 au siku 90,” hizi ni kauli za utawala
wa kibabe, na udikiteta. Hakuna dhana ya utawala bora,” alisema.
Alihoji kuwa kama kosa ni uchochezi,
mbona kuna kesi mahakamani inayomhusu Kibanda na mwandishi Samson
Mwigamba wakidaiwa kuchapisha makala ya uchochezi?
Kwamba kesi hiyo ina utofauti gani na
tuhuma hizi zinazoitwa uchochezi hadi kusababisha magazeti ya Mwananchi
na Mtanzania kufungiwa bila kupelekwa mahakamani?
Dk. Lwaitama alisisitiza kuwa kitendo
kilichofanywa ni kama vile Tanzania hakuna mahakama wakati rais anateua
majaji kila mara, na hivyo kuhoji kazi zao ni zipi kama mawaziri
wanajipangia hukumu.
Wanaharakati
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binadamu (THIRD Coalition), Onesmo Olengurumwa alisema leo wanakutana
na wadau mbalimbali wa habari kwa lengo la kujadili na kutoa tamko
rasmi kuhusiana na suala la kufungiwa magazeti hayo.
Alisema mara baada ya kukutana watazungumza na waandishi wa habari kutoa maazimio waliyofikia katika kikao hicho.
Hata hivyo, alisema sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ni kandamizi na inahitaji kuondolewa.
Olengurumwa aliongeza kuwa sheria zilizopo zinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
“Sheria hii ni kandamizi kwa kuwa
serikali wao ndio walalamikaji, lakini wao wenyewe wanatoa uamuzi bila
kushirikisha upande wa pili, jambo ambalo ni unyimwaji wa uhuru wa
vyombo vya habari,” alisema.
Zanzibar wacharuka
Jumuia ya Waandishi wa Habari za
Maendeleo Zanzibar (Wahamaza) nayo imeungana na watetezi wa uhuru wa
vyombo vya habari kusikitikia uamuzi wa serikali kufungia magazeti ya
Mwananchi na Mtanzania.
Katibu wa Wahamaza, Salma Saidi alisema
uamuzi wa serikali umetolewa wakati wanatasnia ya habari wanadai uhuru
zaidi wa habari, na wakati bado wanalalamikia kufungia gazeti la
MwanaHALISI kwa muda usiojulikana.
“Wahamaza inaamini kuwa adhabu ya
kuyafungia magazeti ni kubwa mno na haikusitahiki, na sababu
zilizotolewa na serikali kuyafungia magazeti hayo hazitoshelezi,”
alisema.
Alisema kuwa wanaamini kwamba njia bora
ya serikali kujenga utawala bora wenye kuheshimu sheria ni kutumia
mahakama katika malalamiko dhidi ya habari zinatolewa na vyombo vya
habari.
“Wahamaza inatoa wito kwa wadau wa
vyombo vya habari nchini kuendelea na harakati za kuitaka serikali
kufuta sheria zote zitazotumia kukandamiza vyombo vya habari ikiwa
pamoja na sheria ya kufungia magazeti,” alisema.
No comments:
Post a Comment