Thursday, April 24, 2014

PICHA NA TAARIFA:BALOZI WA TANZANIA NCHINI MAREKANI NA MEXICO LIBERATA MULAMULA AWAASA WANA DMV KUJITOKEZA KWA WINGI KATIKA SHEREHE ZA MUUNGANO

 Mh.balozi akishauriana jambo na mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika wizara ya mambo ya nje Bi.Mindi Kasiga ambaye atakuwa ndio MC wa shughuli hiyo.
 Mh.Balozi wa Tanzania Marekani na Mexico Liberata Mulamula akizungumzia maandalizi ya sherehe za miaka 50 ya muungano ofisini kwake Washington Dc Jumatano, Aprili 23, 2014.
 Mwenyekiti mwenza wa kamati ya maandalizi afisa ubalozi Suleiman Saleh akijibu maswali ya mabloger wa DMV,kulia kwake ni Dickson Mkama wa Swahili TV

Mh, balozi akijibu maswali kushoto ni Sunday Shomari na kulia kwa balozi ni Mubelwa Bandio wa Kwanza production.
--
Katika mkutano huo na mablogger wa DMV Mh,Balozi Liberata Mula mula amesema maandalizi sasa yamepamba moto ikiwa ndio count down kuelekea D-day (wakihesabu siku zilizobaki kuelekea siku ya kilele cha maadhimisho hayo ya miaka 50 ya muungano wa Tanzania). Mh.balozi ameasa watanzania wa DMV na majimbo ya karibu kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo kwani ni siku ya kihistoria kwa taifa la Tanzania na inafanyika kwa mara ya kwanza Washington Dc.

 Ameeleza kuwa kila kitu kitu kiko tayari na katika siku hiyo ameeleza mtiriririko mzima ambapo sherehe zitaanza asubuhi katika ofisi za ubalozi wa Tanzania Dc ambapo kutakuwa na "Open house " ikiwa na maana maonyesho ya kuitangaza Tanzania ilikotoka, iliko na inakoelekea ikiwa ni pamoja na maonyesho ya mitindo , utalii na mavazi ya mtanzania , shughuli hiyo itaanza saa 4 asubuhi mpaka saa tisa alasiri. Na katika hafla hiyo kutakuwa na vyakula vya aina mbali mbali vya Tanzania kuanzia kifungua kinywa mpaka chakula cha mchana ambapo kutakuwa na vyakula mbali mbali vya Tanzania kama vile mihogo, maandazi, kalmati n.k. 

vitafunwa hivyo vipo zaidi ya aina 22, aidha amesema pia kutakuwa na chakula cha mchana ikiwa utakosa cha asubuhi kama vile pilau, maharage, mihogo ya Nazi n.k. Mchana chakula kitapatikana kati ya saa 7 hadi 8 alasiri pia kutakuwa na vinywaji kutoka Tanzania kama vile Konyagi, bia za Tanzania, Juice na wine ambavyo tayari vimeshawasili. Vyakula hivi ni bila malipo yeyote amesisitiza. Kutakuwa na maonyesho mbali mbali ikiwa ni pamoja na mavazi, mitindo na michezo ya kuigiza.

Na baada ya hapo jioni kuanzia saa mbili usiku kutakuwa na hafla rasmi ya usiku "Tanzania Muungano Night" ambapo wote mnaalikwa bila kukosa na bila kuchelewa katika ukumbi wa Matnice Events and Conference Center 7925 Central Avenue Capital Heights Md 20743. Wageni rasmi ni kutoka pande mbili za muungano ambao Mh. Mwigulu Nchemba (Mbunge na naibu waziri wa fedha na Uchumi Tanzania bara na upande wa Zanzibar atakuwepo Mh. Dr.Mwinyihaji Makame mwakilishi na waziri wa nchi ofisi ya rais ambaye pia ni 

Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Zanzibar na watawasili kuanzia Ijumaa hapa Washington Dc. Wageni kutoka serikali ya Marekani ni balozi Donald Tate Boum naibu waziri wa mambo ya nje anayeshughulikia masuala ya Afrika pamoja na viongozi wa biashara na viongozi wa mabalozi kutoka kila kanda.

Shughuli ya usiku itaanza saa mbili kamili mpaka Liamba ambayo kutakuwa na vyakula vya kila aina kwa ajili yako hakuna kiingilio wala malipo ya chakula ila katika upande wa vinywaji ni mfuko wako tu kunywa unachotaka alisisitiza balozi. Kutakuwa na waigizaji, waimbaji , ngonjera , muziki na kila aina ya burudani na siku ya Jumapili itakamilishwa na kabumbu "Muungano soccer tournament" kuanzia saa tisa alasiri huko Fairland recreational Park 3928 Green castle Rd, Fairland Md 20866.

Timu ya Zanzibar Heroes ya DMV ambayo itapambana na Kilimanjaro stars ya DMV na balozi atafungua mechi hiyo kwa kupiga mpira na ameahidi atafunga goli , aidha Mh.balozi amesema michezo ni mingi ikiwa ni pamoja na kuvuta kambi n.k na kuwaomba wakazi wa DMV na familia zao wajitokeze kwa wingi. Washindi watapata medali na vikombe aliongeza balozi akisema "hamtatoka mikono mitupu na nyama choma ni za kutosha sana zitakuwepo zikiongozwa na wanajumuiya wa DMV wenyewe".

WAZIRI MKUU MSTAAFU CLEOPA MSUYA ASTAAFU SIASA, RAIS JK AMPONGEZA


Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiwa viongozi wengine wakuu wa serikali chama cha Mapinduzi CCM, akiwemo Katibu Mkuu wa CCM Taifa, katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Waziri mkuu wa Tanzania mara mbili katika awamu mbili tofauti, Mzee Cleopa David Msuya (wa kwanza kulia kwa Rais) ambaye amestaafu rasmi siasa baada ya kuitumikia kwa zaidi ya miaka 33.

UTAFITI:WANANCHI WANAUNGA MKONO RASIMU YA KATIBA YA WARIOBA


Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Twaweza umebainisha kuwa wananchi wanaunga mkono kwa kiwango kikubwa Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Ripoti ya utafiti huo uliofanyika Februari, mwaka huu kwa njia ya simu za mkononi na watu kuulizwa kuhusu mchakato wa Katiba, inaeleza kuwa kama wananchi wangeipigia kura rasimu hiyo mwezi huo, Katiba hiyo ingepitishwa kwa asilimia 65 Zanzibar na asilimia 62 Tanzania Bara.

Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi alisema kati ya watu waliohojiwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 20 wangepiga kura ya hapana, kwa upande wa Zanzibar watu ambao wangesema hapana wangekuwa asilimia 19.

“Watu ambao walisema hawana uhakika na hawajui lolote kwa upande wa Zanzibar ni asilimia 19 na Tanzania Bara asilimia 15,” alisema.

“Zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walisema wana nia ya kupiga kura ya kuikubali Katiba (rasimu) kama ilivyo sasa.”

Muundo wa Serikali

Kuhusu muundo wa Serikali, Mushi alisema: “Asilimia 80 ya Wazanzibari wanaunga mkono muundo wa serikali tatu. Kwa Tanzania Bara wanaounga mkono serikali tatu ni asilimia 43.”

Alisema takwimu hizo ni tofauti na zilizotolewa miezi minane iliyopita ilipotolewa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, ambayo asilimia 51 ya wananchi wa Tanzania Bara walipendekeza muundo wa serikali tatu.

Alisema baada ya kutolewa kwa Rasimu mbili za Katiba (ya kwanza na ya pili), Wazanzibari wanataka uhuru zaidi wa kujitawala au muungano wa serikali tatu, huku wananchi kutoka Tanzania Bara wakigawanyika nusu kwa nusu juu ya muundo wa serikali wanaoutaka